Taasisi za haki jinai zatakiwa kuajiri wataalam wa lugha ya alama
MOROGORO: TUME ya Rais ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ambayo kwa sasa imekuwa ni Kamati imeshauriwa kupendekeza kwa taasisi za kijeshi kuweka utaratibu wa kuajiri wataalamu wa lugha ya alama na maandiko ya nukta nundu ili kuwasaidia watanzania wenye matatizo hayo kuweza kuwasiliana na wenzao wa urahisi.
Tume hiyo ambayo kwa hivi sasa imekasimiwa madaraka na kuwa Kamati ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yake kwa taasisi zenye mifumo ya haki jinai ambazo zinakadiriwa kufikia 18.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro mjini Kichama , Fikiri Juma alitoa pendekezo hilo mjini Morogoro wakati wa kongamano lililoandaliwa na Tume hiyo ikiongozwa na Mjumbe wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu ,Balozi Ernest Mangu.
Kongamano hilo liliwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kupata maoni yao juu ya mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo kwa Rais ambalo likilenga kupata maoni juu ya mapendekezo ya kuboresha wa taasisi za haki jinai .
Fikiri katika mapendelezo yake kwa tume hiyo , alishauri ya kwamba kuna haja ya kubadilisha jina la Magereza na kuitwa chuo cha mafunzo ili wafungwa wapate mafunzo badala ya mateso.
Pia alipendekeza ya kwamba Taasisi za kijeshi ziajiri Wataalam wa lugha ya alama na wale wa nukta nundu ili kuwasaidia watanzania wenye matatizo ya kusikia na walioona kuweza kuwasiliana na wenzao kwa urahisi.