Taasisi za serikali zabanwa ukusanyaji mapato

SERIKALI imezitaka wizara, idara zinazojitegemea na taasisi za serikali zinazokusanya mapato yasiyo ya kodi, kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo yake iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Elijah Mwandumbya wakati wa semina ya taratibu za ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi iliyowakutanisha maofisa mipango, Tehama, wahasibu na wakaguzi wa ndani.

Mwandumbya alisema tathmini za hivi karibuni zinaonesha mwenendo usioridhisha wa mapato yasiyo ya kodi kwa wizara, idara zinazojitegemea na taasisi za serikali zinazokusanya mapato hayo ukilinganisha na mapato ya kodi.

“Katika bajeti ya mwaka huu serikali imejipanga kutumia Sh trilioni 41, hivyo ni lazima tuikusanye ili kutekeleza bajeti iliyopitishwa na bunge, mapato hayo ni ya kodi yanakusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na wizara, idara zinazojitegemea na taasisi za serikali,” alieleza.

Alisema licha ya mapato yanayokusanywa na TRA, wizara na idara zinazojitegemea, kiasi kinachobaki katika utekelezaji wa bajeti serikali hukopa mikopo yenye gharama nafuu au mikopo ya kibiashara ambayo ni takribani asilimia 40 ya bajeti yote.

Mwandumbya alisema serikali hufanya uamuzi wa kukopa ili kutekeleza mipango iliyojiwekea ikiwamo ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ikikamilika, hufungua fursa nyingine za kiuchumi kwa sekta binafsi kukua na hatimaye kuzalisha mapato zaidi.

Alibainisha kuwa inapotokea kukawepo eneo ambalo halijafanikiwa katika ukusanyaji wa mapato, hata kama lilipangiwa kiwango kidogo cha mapato, huathiri utekelezaji wa bajeti ya serikali.

Aliwataka wataalamu walioshiriki semina hiyo kuwa chachu kwa wengine katika maeneo yao kwa kuwajengea uwezo ili kuleta ufanisi na kuhakikisha kuwa taratibu stahiki zinazingatiwa katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button