Taasisi zatakiwa kuimarisha huduma kwa wateja

TAASISI mbalimbali za serikali zimeagizwa kufanya maboresho katika utoaji wake wa huduma kwa wateja, ili kuepusha malalamiko na gharama zisizokuwa za msingi kutoka kwa wateja wao.

Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ametoa agiza hilo alipotembelea banda la Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

“Kama serikali inatakiwa tufanye maboresho katika kuhudumia wateja na hili lipo kwenye sekta nyingi sio ninyi tu unaona hata kwenye makazi watu wanajenga makazi holela na hilo linawagusa ninyi na sekta nyingine.

“Kwa hiyo tuwasaidie wananchi, wawekezaji wasitupe fedha zao, muda wao sehemu ambayo sio sahihi,” amesema.

Amesema wawekezaji wengi wanalalamikia baraza hilo kwa urasimu pamoja na kutozwa gharama kubwa, ambapo alitolea mfano mtu anapoanza kujenga kiwanda na baadaye anaambiwa amekosea atoe hapo anakuwa amewekeza fedha nyingi.

Ameshauri NEMC kuona hilo mapema kabla mwekezaji hajaanza ujenzi, ili asipoteze fedha zake, pia kufanya tathmini mapema katika eneo mwekezaji analotaka kujenga ili ajue anachopaswa kukifanya.

“Tulifanyie kazi tuone namna gani ya kuhudumia kwa haraka wawekezaji hawa wasije wakaingia gharama za bure halafu baadaye tukasema hakufuata vigezo vinavyotakiwa,” amesema.

Katika hatua nyingine alipongeza baraza hilo kwa kusimamia changamoto ya kelele iliyokuwepo kutoka kwenye baa, miziki na nyumba za ibada.

“Kwenye kelele nakumbuka mlifanya vizuri sana kupunguza kelele kwa wananchi ambazo zilikuwa ni kero hata kwangu mimi mwenyewe wenye baa, wenye miziki lakini hata nyumba za ibada hilo nashukuru mmefanya kazi nzuri hata wananchi wanaelewa,” amesema.

Awali Ofisa Elimu ya Jamii kutoka NEMC, Suzan Chawe alikiri kupokea maoni na malalamiko kuhusu mambo ya mazingira kisha kuyatafutia ufumbuzi.

“Tunapokea changamoto kutoka kwa wananchi wengi wanalalamika kuhusu kelele, lakini wengine wanalalamika kuhusu ukaribu wa baraza na baadhi ya miradi yao , wengine wangependa kuona gharama zinapungua,” amesema.

Amesema baraza hilo pia limekuwa likiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ili kuwaelimisha wawekezaji anapofika kujua taratibu zipi anapaswa kuzifuata za kimazingira na vibali vya mazingira kabla ya kuanza ujenzi.

Amesema katika maonesho yanayoendelea mkoani Mbeya wamekuwa wakipokea maoni na malalamiko kuhusu mambo ya mazingira, pia wamekuwa wakiwasaidia wawekezaji kujisajili kwa ajili ya kufanya tathmini ya kimazingira kama wataalam elekezi.

Habari Zifananazo

Back to top button