TADB waomba kibali kufungua kiwanda

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), imetuma ombi kwa serikali la kutoa kibali kwa mwekezaji cha kufungua Kiwanda cha kuchakata korosho katika Kanda ya Kusini.

Akitoa ombi hilo  mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, leo Julai 6,2023 katika uzinduzi wa ofisi ya benki hiyo Kanda ya Kusini, Mkurugenzi wa TADB Frank Nyabundege amesema iwapo serikali  itatoa kibali, kitajengwa  kiwanda cha kuchakata korosho kuanzia kwenye kubangua korosho ghafi (RCN), kuzisafisha mpaka kuzifungia kwenye vifungashio na kuzisafirisha nje ya nchi.

Amesema, Kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 1,800 ambazo kati ya hizo asilimia 90 itakua ni wanawake.

Advertisement

“Kiwanda hiki kitakua na uwezo wa kubangua tani 33,000 kwa mwaka na kitaanzisha miradi ya mfano ya kina mama takribani 500 ambao watakopeshwa mashine ndogo ndogo za kubangua na kuchakata korosho na kuzipeleka katika nchi za Marekani na Ujerumani, ” amesema na kuongeza:

“Mh Waziri Mkuu, naomba nimtaje mwekezaji huyu ambaye ni mwanamke mzalendo na mfanyabiashara mashuhuri Sarah Masasi ambae anategemea kuweka kiwanda cha kisasa chenye teknolojia ya kusafisha korosho katika viwango  vya kimataifa mkoani Lindi.

“Tunapopata wawekezaji kama hawa, sisi kama Benki ya Maendeleo tupo tayari kuchagiza mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Amesema, TADB kwenye mnyororo wa thamani wa korosho katika Kanda ya Kusini wamekopesha sh bilioni 35 tangu msimu wa mwaka 2018/2019.

“Mh Waziri Mkuu, tunafahamu kuwa Kanda ya Kusini ni kanda ambayo wakulima wake wamejikita katika kilimo cha zao la korosho, kwa kutambua hilo, sisi kama benki tumelipa kipaumbele zao hili ndio maana tunawekeza fedha nyingi katika zao hilo,”amesema.

4 comments

Comments are closed.