KITENGO cha Huduma za Ajira nchini -TaESA kimeshaanza mchakato wa kuandaa mikataba maalum ya ajira kati ya Tanzania na mataifa mengine kwa lengo la kuongeza fursa nyingi za ajira za nje kwa watanzania.
Akizungumza na Dailynews Digital jijini DSM, Mkurugenzi wa Huduma za Ajira Nchini- TaESA, Joseph Nganga amesema makubaliano ya kuandaa mikataba hiyo yameshaanza ambayo itakuwa ya kudumu kati ya Tanzania na mataifa mengine.
Nganga amesema lengo la kuingia katika makubaliano ya mikataba ni kutaka kulinda haki na maslahi bora ya watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.
Amesema hivi sasa wameanza utaratibu wa kuwaandaa watanzania kwa kuwapatia mafunzo maalum ya kulifahamu soko la ajira la nje ili waweze kufahamu sheria za kazi na wajibu wao katika kazi wanazopangiwa kufanya nje ya nchi.
“ Utaratibu huu umewasaidia watanzania wengi hasa vijana ambao wenye ujuzi na wasio na ujuzi kupatiwa ushauri nasihi kuhusu masuala ya soko la ajira kulingana na utaalamu wao unaofaa” alisema Nganga .
Hatahivyo Kitengo cha Huduma za Ajira nchini TaESA kimeendelea pia kuwahamasisha mawakala wanaoshirikiana na serikali kutafuta ajira za nje kuzingatia masuala ya diplomasia na miongozo ya sheria za kazi utakaoweza kuleta tija kwa watanzania wengi kupata kazi za nje.
Mpaka sasa zaidi ya watanzania laki nne wamesajiliwa ambao wanafanya kazi nje ya nchi na kutambulika katika mfumo wa ajira nchini