Tafiti zabaini aina 47 mimea vamizi

DODOMA; Serikali imesema hadi sasa tafiti zimebaini aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula ametoa kauli hiyo leo Septemba 6, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mohammed Juma Soud aliyehoji serikali ina mpango gani kupunguza upoteaji wa uoto wa asili nchini unaosababisha kupoteza hadhi kwa Hifadhi na Mapori ya Akiba.

“Sababu kubwa ya kupotea kwa uoto wa asili katika Hifadhi na Mapori ya Akiba ni ongezeko la mimea vamizi katika maeneo hayo.

“Mimea hiyo husababisha mabadiliko ya aina ya mimea katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutoa fursa kwa mimea isiyoliwa na wanyamapori kustawi zaidi, kuongezeka na kupunguza uoto wa asili ambao ni tegemeo la wanyamapori.

“Hadi sasa, tafiti zimebaini aina 47 za mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Sababu zinazopelekea kushamiri kwa mimea vamizi ni pamoja na uingizaji wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, mabadiliko ya tabianchi, shughuli za binadamu na viumbepori wahamao,” amesema.

Amefafanua kuwa katika jitihada za kudhibiti mimea vamizi, wizara kupitia taasisi za uhifadhi inatekeleza mkakati wa kukabiliana na mimea vamizi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kwa kung’oa mimea husika katika hifadhi.

“Aidha, mikakati mingine ni kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu, ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini sambamba na kuwekeza zaidi katika utafiti, ili kupata suluhisho la kudumu,” amesema.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button