loader
Dstv Habarileo  Mobile

Kitaifa

Mpya Zaidi

Abiria Tazara anaswa na meno ya tembo ya milioni 26/-

JESHI la Polisi Kikosi cha Reli ya Tazara linamshikilia mtu mmoja aliyekamatwa akisafirisha vipande 14 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 29 na jino moja la Kiboko lenye uzito wa gramu 900, vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 27.9.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi kikosi cha Tazara, Innocent Mugaya alimtaja mtu huyo kuwa ni Ally Juma ambaye anatambulika pia kama Ngangari ambaye alikamatwa Desemba 26, 2013 kwenye treni hiyo eneo la Kisaki Wilaya ya Morogoro.

“Askari wetu wa inteligensia walikuwa ndani ya treni hiyo ya abiria, baada ya kupata taarifa kutoka kwa msiri wetu, walimkamata mtu huyo akiwa amebeba meno ya tembo kilo 29 pamoja na jino moja la kiboko, begi moja likiwa na vipande vinane na jingine vipande saba,” alisema Kamanda Mugaya.

Kamanda huyo alisema baada ya kufika maofisa kutoka wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii walibaini vipande hivyo 14 ni vya meno ya tembo na jino moja la kiboko.

“Vipande 14 vya meno ya tembo ni sawa na tembo saba waliouawa na thamani yake ni Sh 25,520,000 aidha jino moja la kiboko ni sawa na kiboko mmoja aliyeuawa na thamani yake ni sawa na Sh 2,400,000,” alisema Kamanda Mugaya.

Aidha alisema askari hao pia walikamata bangi kilo 19 ikiwa kwenye mabegi mawili yaliyotelekezwa na watuhumiwa au mtuhumiwa ambaye hajafahamika na thamani yake pia haijafahamika.

Alisema askari wa Tazara wanajitahidi kuzuia uhalifu ambao unafanyika katika treni hiyo ikiwa ni pamoja na wahalifu wanaosafirisha nyara za Serikali kupitia treni ya Tazara ambao wanawaua wanyama wanaoingizia Serikali fedha nyingi kupitia sekta ya utalii.

Aliwataka abiria wote wanaotumia treni hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kutoa taarifa ili kutokomeza uhalifu na ujangili unaoikosesha Serikali mapato.

zaidi ya miaka 6 iliyopita