loader
Dstv Habarileo  Mobile

Kitaifa

Mpya Zaidi

Chuo feki kilichotelekeza wanafunzi chafungwa rasmi

SAKATA la uwepo wa chuo bandia cha Kilimo na Mifugo cha Nice Dream kilichopo Ilemi jijini Mbeya, limechukua sura mpya baada ya serikali na ofisi ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), kukifunga rasmi chuo hicho, huku wanafunzi wakiamriwa kurejea makwao ndani ya siku tatu.

Aidha, mmiliki wa chuo hicho anasakwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuwatapeli fedha wanafunzi zaidi ya 46 kutoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwamo Kagera (41), Mara (2), Mbeya (2) na mmoja kutoka Dar es Salaam.

Mamlaka hizo zimechukua jukumu la kufunga chuo hicho, kutokana na kutosajiliwa huku uongozi wake ukiwa umetajwa kutapeli wanafunzi hao zaidi ya Sh milioni 26, ambazo zilikuwa sehemu ya ada wakati wa kuanza chuo Septemba mwaka huu, kabla ya hivi kutelekezwa na uongozi wa chuo na hata kujikuta wakikosa chakula, kiasi cha wenzao kuzirai kwa njaa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigalla juzi aliwakilishwa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya, Quip Mbeyela kufika chuoni hapo na kutoa tamko la Serikali la kufunga chuo hicho na kuwaamuru wanafunzi kurejea makwao ndani ya siku tatu.

Mbeyela alisema uongozi umefikia uamuzi huo, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wanafunzi wakidai kuwa mwenye chuo amewatapeli na kutoweka kusikojulikana, akiwa amewaacha bila huduma zozote, zikiwemo za masomo na chakula.

Alisema baada ya hapo walichukua uamuzi wa kuripoti tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Mbeya, ambako wamefungua jalada la utapeli. Pia walimkamata aliyekuwa Msimamizi wa Ofisi (Katibu Muhtasi), Shakira Siraji ambaye alihojiwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Akizungumza na wanafunzi na majirani wanaowahudumia wanafunzi hao kwa chakula, mwakilishi huyo wa mkuu wa wilaya alisema wanafunzi wanapaswa kurudi makwao ndani ya siku tatu na hawastahili kuwepo hapo baada ya siku hizo kumalizika.

Wakati huo huo, Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilitoa msaada wa chakula cha siku tatu chenye thamani ya Sh 300,000 zikiwemo kilo 100 za mchele, maharage, mafuta na chumvi, visaidie wanafunzi katika kipindi hicho walichopewa wakati wakiwasiliana na wazazi na walezi wao ili wawatumie nauli.

Kabla ya kuondoka eneo la chuo hicho, Kaimu Katibu Tawala alisema hatua za kisheria zitaendelea. Alichukua orodha ya majina ya wanafunzi wote waliotapeliwa pamoja na mawasiliano ili upelelezi wa kisheria ukikamilika, wapewe haki zao wakati jeshi la polisi likiendelea kusaka wahusika wa utapeli huo.

Msajili wa Vyuo vya Ufundi (Nacte) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Alex Nkondola, ambaye alifika chuoni hapo jana, alisema wao ndiyo wenye jukumu la kusajili vyuo kisheria, lakini Chuo cha Nice Dream hakijasajiliwa na hakina sifa za kusajiliwa.

Alisema kwa ujumla kimekosa sifa ya kupokea wanafunzi na kusema uongozi umekiuka sheria na utaratibu wa kuwa na wanafunzi.

Alisema hatua zinazopaswa kufuatwa hivi sasa ni dola kuachiwa jukumu la kumtafuta mmiliki wa chuo na kuendelea na uchunguzi, kubaini wengine wanaohusika, kutokana na wanafunzi kudanganywa kuwa ni chuo cha Serikali, huku kikidanganya kuwa kilizinduliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alikana kukitambua.

Hata hivyo, wanafunzi walionekana kutoridhishwa na uamuzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Nacte wa kukifunga chuo hicho na kuwataka warudi kwao, wakisema uamuzi huo hautoi suluhisho kwao, kutokana na utapeli wa mamilioni ya fedha waliofanyiwa.

zaidi ya miaka 5 iliyopita