loader
Dstv Habarileo  Mobile

Kitaifa

Mpya Zaidi

Wasichana waongoza mapenzi umri mdogo

IDADI kubwa ya vijana hususan wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaanza mapenzi katika umri mdogo hivyo kujiweka katika hatari ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Hayo yamo katika mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ya VVU kwa vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.

Ofisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/Ukimwi kutoka UNESCO, Herman Mathias, akiwasilisha mada hiyo amesema hadi sasa kuna asilimia 3.9 ya wasichana wenye umri huo wamepata maambukizi ya VVU ikilinganishwa na asilimia 1.7 ya wavulana.

Aidha alisema kufanya mapenzi katika umri mdogo pia kunachangia kwa kiasi kikubwa mimba za utotoni na kuathiri ustawi wa maisha ya wasichana. Amesema kwa wastani watoto wa kike 6,000 huachishwa masomo kila mwaka kutokana na mimba za utotoni.

“Wasichana wengi wamekatishwa masomo kwa ajili ya kupata mimba za utotoni zinazochangiwa na kufanya mapenzi katika umri mdogo tabia ambayo pia inachangia pia maambukizi ya VVU”, alisema Mathias.

Alizitaja tabia nyingine hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ni kitendo cha kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja, kuwa na wapenzi wenye umri mkubwa na ngono wenzi.

Nyingine ni matumizi duni na yasiyo endelevu ya kondomu, kufanya ngono wakati umelewa, ngono kinyume na maumbile na ngono ya jinsia moja.

Akichangia suala hilo, Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Rose Haji Mwalimu amesema tamaduni zinazoendelezwa katika jamii pia zinachangia kumweka msichana katika kundi hatarishi la kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Amezitaja tamaduni hizo kuwa pamoja na kumbagua mwanamke katika majukumu mbalimbali kijinsia kutokana na tabia inayofundishwa na kutolewa kwa mtu kulingana na jinsi yake.

Amewataka wanahabari vijana kuhakikisha kuwa wanahamasisha kubadilisha tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambazo zimemzunguka mwanamke. Baadhi ya mifano alisema ni mitala.

Mahusiano ya kimapenzi hata katika jamii isiyokumbatia mitala kutoka na tamaduni zilizojikita katika jamii inakubalika kwamba mwanaume ana haki ya kuwa na wapenzi wengi wakati wanawake wanatakiwa kuwa waaminifu kwa mtu mmoja ambao ni waume zao.

Kutokana na tamaduni hizo yanajengwa mazingira ambayo mwanamke anakuwa hana uwezo wa kujadili masuala ya ngono salama au ya kuridhisha kwa sababu kunakuwa hakuna mawasiliano katika nyumba kuhusu ngono kati ya mume na mke.

Mradi wa SHUGA Redio unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika ya Kimataifa moja linaloshughulikia Huduma za Watoto (UNICEF), Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Redio Jamii 10 nchini Tanzania una lengo la kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Redio hizo ni kutoka Karagwe, Kahama, Kyela, Kitulo na Kwanza Jamii. Nyingine ni kutoka Iringa, Simanjiro, Ifakara, Sengerema na Uvinza.

zaidi ya miaka 6 iliyopita