loader

Makala

Mpya Zaidi

Fursa za biashara Zanzibar

MACHI 16 mwaka huu, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha gazeti hili, Daily News na SpotiLeo iliandaa Jukwaa la Biashara Zanzibar katika mkakati wake wa kutangaza fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi Bara na Visiwani.

Jukwaa hilo ni la tano kuandaliwa na TSN, mengine yakiwa yamefanyika kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Tanga huku miji ya Arusha na Geita ikitajwa kwamba ndiyo itafuatia.

Katika kuandaa Jukwaa la Zanzibar TSN ilipata ushirikiano mkubwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Baraza la Biashara Zanzibar.

Mbali na mawaziri kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), lilihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Kwa upande wa SMZ mawaziri waliohudhuria ni Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahamoud Thabit Kombo na wengineo. Viongozi wengine waliohudhuria ni Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu na wajumbe zaidi ya 350 wakiwemo kutoka kampuni kubwa 50.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alidokeza kwamba, mbali na Zanzibar, TSN imeanza mikakati ya kufanya majukwaa hayo nje ya nchi ikilenga kutangaza fursa zilizopo nchini na kwamba tayari wameanza mawasiliano na nchi ya Oman.

“TSN katika kuangalia fursa za kibiashara zilizopo Zanzibar waandishi wa habari wamekaa katika visiwa hivi kwa wiki mbili wakiangalia fursa zilizojificha na kuzitangaza katika magazeti na kwenye mitandao ya kijamii,” anasema Dk Yonazi.

Mwenyekiti wa bodi ya TSN, Hab Mkwizu anasema mpango huo ulibuniwa mwaka jana na TSN ili kuibua fursa mbalimbali za uchumi katika mikoa na kuhamasisha wananchi wa maeneo hayo kutumia fursa hizo kujiletea maendeleo yao binafsi na taifa.

“Katika kutekeleza mpango huu TSN imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ambao ni pamoja na taasisi za umma na asasi binafsi,” anasema.

Mwenyekiti wa bodi anasema mwitikio wa majukwaa haya katika mikoa iliyofanyika umekuwa mzuri sana na uhitaji wake unaongezeka kila siku na kwa sasa kuna maombi ya kuendesha majukwaa hayo karibu katika kila mkoa yote na kwamba TSN imejipanga kwenda kote huko.

Anasema huo ni mwendelezo na siyo mwisho wa juhudi za TSN kusukuma maendeleo ya Zanzibar na wataendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali katika kusaidia maendeleo kwa kuibua fursa katika sekta mbalimbali. Katika wiki mbili za kuangalia fursa zilizopo Zanzibar pamoja na mijadala ya siku ya Jukwaa, fursa mbalimbali zinazohitaji uwekezaji zilijitokeza.

Utalii Utalii ni sekta inayoongoza kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ikichangia kwa asilimia 30. Utalii unaotoa ajira kwa wananchi unatokana na visiwa hivyo kuwa na fukwe za kuvutia, historia ya mambo ya kale kutokana na Zanzibar kuwa eneo lenye historia mbalimbali za kale na mji mkongwe.

Zanzibar pia ina hifadhi ya taifa ya Jozani–Ghuba ya Chwaka iliyopo katika mkoa wa Kusini Unguja ikiwa na kima punju wanaopatikana zaidi katika hifadhi hiyo.

Ingawa hifadhi ina ukubwa wa hekta 5,000 zinazotumika kwa sasa hekta 20 pekee hivyo bado kuna fursa za uwekezaj hifadhini humo.

Historia ya Zanzibar inaanzia mwaka 1500 na hivyo kuna asilimia 80 ya mambo ya kale katika visiwa hivyo ambayo hayajatangazwa ipasavyo.

Halikadhalika utalii wa utamaduni ikiwemoo vyakula kama vile urojo, magari ya chai maharage, muziki wa taarabu na ngoma za asili ni vitu ambavyo havijatangazwa ipasavyo.

Katika utalii wa baharini bado kuna fursa nyingi ikiwemo maeneo ya fukwe kwa ajili shughuli mbalimbali, utalii wa uvuvi na mengineyo.

Upo pia utalii wa vipepeo, kasa na viumbe vingine vinavyopatikana Zanzibar pekee. Ujenzi Kutokana na uhaba wa makazi kuna fursa nyingi za ujenzi katika visiwa hivi.

Pia kuna fursa za ujenzi wa hoteli, kumbi za shughuli mbalimbali, ofisi na kadhalika. Katika mkoa wa Mjini Magharibi kuna mpango unaoshirikisha Benki ya Dunia unaolenga katika ‘uboreshaji wa mji wa Zanzibar’ na tayari miongozo imetengenezwa.

Katika eneo hilo wananchi wako tayari kupisha uwekezaji na baadaye kwa makubaliano maalumu wakirudi watapatiwa makazi katika ghorofa mbili badala ya moja wanayoishi sasa na eneo lililobaki mwekezaji atauza.

Pia kuna eneo jipya la uwekezaji lililotengwakatika eneo la Fumba ambapo mpaka sasa ni wawekezaji wachache waliolichangamkia akiwemo mfanyabiashara maarufu, Said Bakhressa kupitia kampuni yake ya Union Group. Serikali pia ina hisa katika uwekezaji huo ambao unashirikisha pia mwekezaji mwingine kutoka Ujerumani.

Uchache wa nyumba za makazi na za kulala wageni, kunafanya upangaji au gharama za nyumba za wageni kuwa kubwa hali inayoonesha kuwa kuna fursa katika eneo hilo zinazoita watu kuzichangamkia.

Kodi ya pango kwa nyumba inafikia hadi Sh 350,000 kwa mwezi huku gharama ya vyumba vya kulala wageni katika gesti za kawaida zikiwa kati ya Sh 40,000 na 50,000.

Viwanda

Katika sera ya kukuza viwanda vilivyokufa kuna fursa za kuongeza thamani ya mazao mbalimbali yanayopatikana visiwani humo. Mazao hayo ni mwani wenye uwezo wa kutengeneza bidhaa zaidi ya 40 ikiwemo sabuni, shampuu na nyinginezo.

Bado kuna hitaji la ujenzi wa viwanda vya kuongeza ubora wa mazao yatokanayo na bahari kama vile kusindika samaki na bidhaa nyingine.

Kuna maeneo maalumu yametengwa kwa ajili ya viwanda na sasa kila wilaya inaangalia aina ya viwanda kulingana na rasilimali zilizopo.

Kuna fursa pia ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani katika mazao ya viungo yanayopatikana kwa wingi katika visiwa hivyo. Zanzibar pia inahitaji viwanda vya dawa na vipodozi vinavyotokana na mazao yanayolimwa Zanzibar. Viwanda vya kemikali zinazotumia chumvi pia vinahitajika visiwani humo.

Kilimo Zipo fursa za kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kilimo kama karafuu, mwani na bidhaa za viungo. Zanzibar inatajwa kuwa mzalishaji wa tatu kwa ukubwa duniani wa zao la mwani.

Uwekezaji ili kuzalisha zaidi wa zao hilo bado unahitajika. Katika mazao ya viungo kuna fursa kubwa ya kufanya kilimo hai kwenye mazao kama pilipili hoho, pilipili manga, iriki, mdarasini, karafuu, tangawizi na mengineyo. Kutokana na ufinyu wa aradhi katika visiwa hivyo, kunahitajika sana kilimo hifadhi, yaani kinachotumia eneo dogo na kutoa mazao mengi.

Mazao ya bahari Dagaa wa Zanzibar wamekuwa na soko kubwa katika nchi mbalimbali kama vile Kenya, Malawi na Comoro. Fursa nyingine ni uzalishaji wa chumvi, ufugaji pweza na ngisi, samaki pamoja na majongoo ya baharini.

Shghuli za kijamii Zipo ajira katika sekta ya utalii kutokana na wanaotafuta kazi wengi hawajakidhi elimu inayotakiwa. Kwa upande wa utoaji huduma mbalimbali ikiwemo usafiri, bado kuna bodaboda chache visiwani humo kulinganisha na maeneo ya Bara.

Bado kuna fursa za utoaji huduma za chakula katika maeneo mbalimbali, vyoo vya umma na masoko kwa ajili ya bidhaa zinazopatikana kwa wingi visiwani humo hususani viungo, karafuu, matunda na ubuyu. Fursa nyingine ni ujenzi wa hospitali binafsi, shule, shughuli za ujasiriamali kwa ujumla na uchoraji kwa kutumia hina.

Benki Katika mjadala kwenye jukwaa la Zanzibar ilibainika bado kuna fursa kubwa ya kufungua mabenki kutokana na mengi kutokuwa na matawi au benki hizo kutofikakabisa visiwani. Ujenzi wa benki zaidi visiwani unatarajiwa kutaleta ushindani utakaosaidia kutoa mikopo kwa wananchi kwa riba nafuu na hivyo kukuza pato la wananchi.

Usafiri baharini Visiwani humo pia kuna fursa za kuwekeza katika vyombo vya usafiri wa baharini kwani vingi hujaza lakini hatua hiyo itaongeza ushindani utakaosaidia huduma kuwa bora zaidi.

Wadhamini wa Jukwaa Jukwaa hilo la Zanzibar lilifanikiwa kutokana na udhamini wa benki ya NBC, Benki ya Azania, Benki ya NMB, benki ya watu wa Zanzibar (ZPB), Mfuko Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma, Nishati na Maji Zanzibar (ZURA) na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Wadhamini wengine ni Nabaki Afrika, kampuni ya VIGOR Group, Hoteli za The Dream, The Africa House Hotel, Park Hyatt Hotel, Mfuko wa barabara Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Tanzania (Ewura).

Wadhamini wengine wa Jukwaa hilo lililofana ni Bohari ya Dawa (MSD), Watumishi Housing Corporation (WHC), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wengineo.

miezi 5 yaliyopita