loader

Makala

Mpya Zaidi

Kituo cha ushauri BRAC kinavyoinua wakulima Butiama

Moja ya mashamba yaliyotokana na msaada wa Brac.WAKULIMA na wafugaji katika Wilaya ya Butiama mkoani Mara ni miongoni mwa wananchi walionufaika kiuchumi kutokana na kupokea ushauri wa mafunzo ya kilimo, mifugo, maji na mazingira kutoka kwenye Kituo cha Mafunzo na Ushauri wa Kilimo cha Buhemba kinachomilikiwa na Kanisa la Kianglikana,(BRAC).

Kituo hicho kimetoa msaada huo kwa wakulima baada ya kupokea misaada ya fedha zipatazo Sh milioni 370 kutoka za Uholanzi, Australia na Uingereza.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kilimo zinazolenga kuinua uchumi wa wananchi katika Wilaya ya Butiama. Meneja wa Kituo cha BRAC, Ezekiel Kabwe, anasema fedha hizo zimetolewa na wabia wa maendeleo toka nchi hizo tatu ambao wamekuwa wakikisaidia kituo hicho kila mwaka kwa lengo la kuwainua kiuchumi wananchi wanaokabiliwa na umasikini uliokithiri katika jamii mbalimbali za Watanzania.

Kabwe anasema fedha hizo zinaendelea kutoa huduma kwa wakulima katika vijiji 21 vya wilaya hiyo katika kuboresha kilimo bora, hifadhi ya mazingira, mifugo, kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama sanjari na kushughulikia ustawi wa watoto wanaofanyishwa kazi katika migodi mbalimbali ya madini.

“Hawa ni wabia wetu wa maendeleo kwa muda mrefu sasa ambao tunaendelea kushirikiana nao na ufadhili wao umeleta maendeleo na mafanikio makubwa kwa wananchi waliokubali kwa nia moja kutekeleza kwa vitendo utekelezaji wa misaada wanayoipata toka kwa wahisani kupitia kituo hiki.

Kituo kunufaisha wengi

“Mwanzoni wakati tunaanzisha kituo hiki ilikuwa ni jambo gumu kuwashawishi wakulima na wafugaji jinsi gani ambavyo wangeweza kunufaika na misaada ya kituo hiki lakini walipoona wenzao wamethubutu sasa wanakiona kituo kama mkombozi wa maendeleo yao katika sekta mbalimbali za kiuchumi,” anasema Kabwe.

Anafafanua kwamba wakulima wanafaidika na misaada hiyo kwa kuendelea kupewa elimu ya mbinu bora za kilimo, matumizi ya mbegu bora ambapo vikundi vya wakulima vimewezeshwa kupata mbegu bora za mahindi, muhogo, alizeti na viazi na kwamba jamii imekuwa pia ikihamasishwa kutunza mazingira kupitia kamati za mazingira na vikundi vya kuotesha miti.

Mzee Patrick Oloo, mkazi wa Kijiji cha Taramanka, Kata ya Sirori Simba ni miongoni mwa mashuhuda wa maendeleo walionufaika na misaada toka kituo hicho cha ushauri na mafunzo ya kilimo cha Buhemba ambaye kutokana na ufugaji wa nyuki sasa ameweza kukuza uchumi wa familia yake kupitia kikundi chao cha Kilimo Mseto.

Mzee Oloo anasema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2006 ambapo kilianza na wanachama 26 lakini kutokana na hali ya kuhama kwa watu toka eneo moja hadi jingine kwa lengo la kutafuta hali nzuri ya kipato wamejikuta wakipungua na kubakia wanachama watano tu ambao wanaendesha shughuli za kikundi hicho.

Anasema BRAC iliwapatia mizinga ya kisasa 22 ya nyuki, wakaanza kuifuga lakini kutokana na wanyama waharibifu kama vile nyani na tumbili kuharibu mizinga hiyo wakati wakifuatilia kula asali sanjari na wizi unaofanywa na binadamu wamebaki na mizinga 16 ambayo inawaingizia kipato cha wastani kati ya Sh laki moja hadi mbili kwa mwaka kwa kila mzinga.

Kituo chenyewe ni soko

“Asali tunayoivuna tunaiuza katika Kituo cha BRAC kwa bei ya Sh 6000 kwa lita moja hivyo utaona kuwa hatuna shida ya soko. Vilevile faida nyingine tunayoipata mbali na kipato cha kutusaidia kutunza familia, nyuki wanatumika kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuwa palipo na mizinga hiyo hakuna mtu anayesogea kukata miti hovyo na hii inatokana na hofu ya kushambuliwa na wadudu hao hatari,” anafafanua Oloo.

Anatanabaisha kwamba ufugaji wa nyuki umekisaidia kikundi chao cha Kilimo Mseto kufungua chama cha kuweka na kukopa (SACCOS) kinachowapa fursa ya kukopeshana kwa riba nafuu.

Akielezea tofauti ya ufugaji wa mifugo kama vile ng’ombe na mbuzi ukilinganisha na nyuki, Mzee Oloo anasema ufugaji nyuki ni nafuu sana kwa kuwa nyuki hawana gharama za utunzaji na wala hawako katika hatari ya kushambuliwa na magonjwa kama ya mifugo na hivyo anawashauri watu wengine wajiunge katika ufugaji huo.

Kikundi kingine kinachofaidika na misaada ya BRAC ni cha Umoja kilichoko katika kijiji cha Kibubwa, Kata ya Butuguri wilayani Butiama. Mwajuma Mirumbi ambaye ni mhudumu wa mifugo katika kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka 2010 anasema kwa sasa kina wanachama 75 wanaojishughulisha na ufugaji wa mbuzi wa maziwa, samaki, nyuki, kilimo cha mibono na utengezaji wa sabuni.

Anasema kikundi chao pia kinashiriki katika utunzaji wa visima vya maji. Mirumbi anasema kutokana shughuli hizo za kiuchumi zinazofanywa na kikundi chao wanafaidika na kuongeza kipato cha familia ikiwa ni pamoja na kuweza kuwalipia ada watoto wao wanaosoma shule za msingi na sekondari tofauti na miaka ya nyuma kabla ya kuunda kikundi hicho.

Anasema mbolea ya samadi na maziwa vinavyotokana na mbuzi vimewaongezea kipato katika kikundi chao kwa kuuza bidhaa hizo kwa wananchi.

Mkopo wa mbuzi 400

Anasema BRAC imewawezesha kupata mkopo wa mbuzi wapatao 400 wenye thamani ya Sh milioni 4.2 waliowapokea ndani ya miezi minne ya awamu ya kwanza ya mkopo huo kabla ya kuongezwa mbuzi wengine wa maziwa 17 wenye thamani ya Sh milioni 2.5 ikiwa ni wastani wa Sh laki moja na nusu kwa kila mbuzi.

Kauli hiyo ya mhudumu huyo wa mifugo wa kikundi cha Umoja toka kijijini Kibubwa inaungana na kauli ya Meneja wa BRAC, Kabwe kuhusiana na ukopeshaji wa mbuzi katika kaya 420 kwa mtindo wa kopa mbuzi, lipa mbuzi. Kabwe anasema hatua imewezesha wananchi kufuga mbuzi wa maziwa na kujipatia vipato vikubwa.

Maziwa hayo anasema yamekuwa pia chanzo cha lishe na kuisaidia jamii katika kupambana na utapiamlo, hususan kwa watoto katika wilaya hiyo ya Butiama.

Uchimbaji wa visima Kuhusu tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama ambao bado ni kero kwa wananchi wengi, hususan waishio vijijini ambao wamekuwa wakihangaika kupata huduma hiyo muhimu kwa tabu ikiwa ni pamoja na wanawake kutembea saa nyingi njiani kutafuta maji, Kabwe anasema hadi sasa kituo chake kimetumia jumla ya Sh milioni 161 kuchimba visima virefu 7 katika vijiji saba.

Anasema hatua hiyo imeondoa tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo ya maji na kuongeza kwamba mipango inaendelea ili kumaliza tatizo kama hilo katika vijiji 14 vilivyobakia vinavyohudumiwa na kituo hicho. Kwa upande wake, Mwajuma Mirumbi anakiri kwamba kijiji chao cha Kibubwa ni miongoni mwa vijiji saba vilivyopokea msaada wa visima viwili vya maji vyenye thamani ya Sh milioni 59 ambapo nguvu za wananchi ilikuwa Sh milioni 15 huku BRAC ikitoa Sh milioni 44.

“Kama kuna jambo ambalo tumepata mwarobaini wake ni suala la msaada wa visima vya maji toka BRAC maana kama ujuavyo ilikuwa ni kero kubwa hapa kijijini na hasa sisi wanawake ambao ndo wenye kuwajibika kutafuta maji kwa ajili ya familia zetu. Tunashukuru sasa tatizo hilo limekwisha baada ya Kituo cha BRAC, Buhemba kutupatia msaada huo,” analiambia jopo la wanahabari waliofika kijijini hapo kujionea hali halisi.

Msaada huo haukuishia Kibubwa pekee bali jopo la Waandishi wa Habari lilifika katika Kijiji cha Biatika Kata ya Buhemba wilayani Butiama na kukutana na kikundi cha Wapanda Miti na kuzungumza na mmoja wa wanachama kikundini hapo, Emmanuel Jozamu ambaye anashukuru msaada huo wa kuchimbiwa kisima mwaka 2007 kinachozinufaisha kaya 170 za kijiji hicho.

Jozamu anasema licha ya kila kaya kuchangia Sh 1,500 tu kwa mwezi huku wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 wakipata maji hayo bila kuchangia, anaelezea umuhimu wa kuwepo kwa kisima hicho kuwa kimewawezesha kupata maji safi na salama tofauti na miaka ya hapo awali waliyokuwa wakisotea kupata maji umbali mrefu tena yasiyo safi na salama.

Mradi wa bajaji

Misaada hiyo ya nchi tatu wahisani kupitia kituo hicho cha Buhemba chini ya Kanisa la Kianglikana Jimbo la Mara imewagusa pia wananchi wa Kijiji cha Busegwe ambapo kikundi chao kiitwacho Muungano kimepata Sh milioni 1.8 zilizotumika kununua bajaji ya kukodisha mwaka 2008 lakini mtaji wao umekua na kufikia Sh milioni 4 sasa.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Richard Ruhutaa anasema fedha hizo zimewasaidia kukopeshana miongoni mwao wanakikundi lakini cha kuvutia zaidi ni mpango wa kusaidia wanachama wake 24 kujenga nyumba bora za kuishi ambapo kikundi kinatoa mabati ya kuezeka nyumba inayokuwa imejengwa na mwanachama wa kikundi hicho.

“Kwa hili tuko makini sana. Hatutoi fedha kwa mwanachama kununua mabati bali tunatoa mabati baada ya kuona hatua ya upauaji imekamilika. Mpango huu umetufanya tuondokane na nyumba za miti na nyasi na kupata nyumba bora kabisa.

“Mbali na mradi wa kukopeshana kwa lengo la kuinua hali za maisha katika familia zetu, tunayo miradi mingine ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa wapatao 50 na kumi kati yao tulipewa na kituo cha BRAC na wengine 40 ni michango ya wananchama. Kikundi chetu pia kina mradi wa ufugaji samaki na tumeshapandikiza samaki zaidi ya 750 katika bwawa la kikundi,” anasema Mwenyekiti huyo.

Kituo cha BRAC kimewawezesha hata wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha mboga na matunda katika kuinua hali zao za maisha kiuchumi na hili linadhihirishwa katika Kijiji cha Rwamkoma kilicho katika Kata ya Butiama kuliko na kikundi cha vijana waliobobea katika kilimo cha aina hizo za mazao.

Kutoka Sh 10,000 hadi mamilioni

Moses Kikama ni kiongozi wa kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka 1999 kikiwa na wanachama sita kwa mtaji wa Sh 10,000 pekee. Anasema kutokana na bidii zao za kuthamini na kukiona kilimo kama uti wa mgongo wa maisha yao, kipato chao kimekua mwaka hadi mwaka na kupata wastani wa pato la kati ya Sh milioni 3 na milioni 4 kila wanapovuna mazao yao ndani ya miezi 6.

“Kwa sasa hivi huwezi kunishawishi nibadilishe aina ya kazi zaidi ya kilimo hiki cha mbogamboga na matunda ambacho kimenisaidia kupata maisha bora na kama mnavyoona hii nyumba nimeijenga kutokana na fedha za kilimo. Hata kuku zaidi ya 400 ninaofuga hapa nyumbani wametoka humo humo kwenye kilimo cha mboga mboga,” anasema Kikama.

Anasema kuwa bidii ya kazi na msaada wa wataalamu toka Kituo cha BRAC, Buhemba ni miongoni mwa sababu za kukua kwa uzalishaji wa mazao hayo katika kikundi chao kilichokua kwa kasi toka mtaji wa Sh elfu kumi mwaka 1999 lakini sasa hivi wanazungumia mamilioni ya pesa.

Katika hatua nyingine, Meneja wa BRAC anasema kituo hicho pia kimeamua kuwapatia mafunzo ya kilimo kwa muda wa mwaka mmoja watoto 45 waliokuwa wakikabiliwa na ajira mbaya kwenye migodi ya madini iliyopo wilayani humo kinyume na Tamko la Umoja wa Mataifa la mwaka 1989 juu ya haki za watoto, lililoridhiwa na Tanzania mwaka 1990.

Anasema tamko hilo baadaye lilitungiwa sheria ya watoto Namba 21 ya mwaka 2009. Lengo la mafunzo hayo anasema ni kuwajengea uwezo wa kujitegemea watoto hao kupitia sekta ya kilimo.

Mwandishi wa mkala haya ni mchangiaji katika gazeti hili.

zaidi ya miaka 5 iliyopita