loader

Makala

Mpya Zaidi

Wengi walaani ukatili wa ‘mtoto wa boksi’

Mariam Said (kati kati) akisindikizwa na askari polisi kwenda kituoni, baada ya kutoa maelezo kwa Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu (hayupo pichani) akituhumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa mtoto wa mdogo wake aliyefariki na yeye kuteuliwa kumlea lakini akawa anamfungia ndani ya boksi. (Picha zote na John Nditi).“NIMEJIKUTA machozi yananitoka baada ya kusoma hiyo habari. Kila nikijizuia yanatoka. Ninamhurumia huyo mtoto huku nikifikiria pia wanangu endapo nitafariki dunia na watakutana na ukatili kama huu,” anasema Shaibu Mohamed, baada ya kusoma gazeti hili kuhusu habari za mtoto aliyekuwa anafungiwa kwenye boksi zaidi ya miaka mitatu na mama yake mkubwa.

“Hili pia ni funzo kwa nyinyi wanaume. Ni lazima mtu uwe karibu na mwanao wakati wote,” anasema mwanamke mwingine anayejitambulisha kwa jina moja la Stellah.

Habari ya mtoto huyo (jina linahifadhiwa) zilizotikisa nchi mwishoni mwa wiki zimewashitua watu wengi na ambao wameishia kulaani kitendo hicho na kumuomba Mungu ampe afya njema, elimu na kila zuri mtoto huyo katika maisha yake ya baadaye.

Elizabeth Francis na Sharrifa Abdallah wakazi wa Mjini Morogoro, wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasema vitendo vya ukatili kwa watoto lazima vipigwe vita na kukomeshwa ndani ya jamii.

Hata hivyo, wamewapongeza wananchi wa mtaa wa Azimio katika Kata ya Kiwanja cha Ndege kwa ujasiri wao wa kufichua tukio hilo na kutaka wengine wenye kuyajua matukio maovu dhidi ya watoto, wayafichue mara moja ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Mkazi wa Kata ya Misufini, Manispaa ya Morogoro aliyejitambulisha kwa jina moja la Sheyla, mbali na kusikitishwa na kitendo hicho cha kikatili dhidi ya mtoto huyo, anashauri adhabu kali zichukuliwe kwa wahusika akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo.

“Haiji akilini kuona baba mzazi wa mtoto anashindwa kuwajibika kwa mwanawe hata kama anaishi na mama yake mkubwa... Alipaswa kufuatilia kila hatua ya malezi ya mwanawe na si kuwaachia walezi hao pekee na kusahau,” anasema mwanamke huyo. “Hiki ni kitendo cha kinyama na kisichokubalika... Hakina budi kilaaniwe na kila mtanzania, lakini uwajibikaji kwa mtoto ni jukumu la mzazi, baba wa mtoto na jamii kwa ujumla. Baba mzazi na baba mlezi hawawezi kukwepa mkono wa sheria katika tukio hili,” anasema.

Joseph Mkude, yeye anasema kama mama huyu hakuwa na nia ya kumlea mtoto huyo angelimwambia mumewe amrudishe kwa baba yake mzazi, kwani kitendo alichokuwa anafanya ni cha uuaji na ukatili wa hali ya juu.

Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro kupitia Ofisa Mkuu wa Mkoa, Oswin Ngungamtitu, anaomba ushirikiano na wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuwafichua watoto wanaofanyiwa unyanyasaji na ukatili hata kama haujapindukia mipaka kama aliokuwa akifanyiwa mtoto huyo.

Hata hivyo, anawaomba wadau mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa wa Morogoro kujitokeza kumsaidia mtoto huo kwa hali na mali ili aweza kuhudumiwa kwa matibabu na chakula. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mtoto huyo alikuwa anafungiwa ndani tangu akiwa na umri wa miezi mitatu, wakati anaishi na mama yake mlezi, Mariam Said.

Mariam alimchukua mtoto huyo kutoka kwa shemeji yake baada ya mdogo wake aliyemzaa kufariki dunia, akimwacha mtoto huyo akiwa na umri wa miezi mitatu. Mariam anaishi na mumewe, Mtonga Omary ambaye ni mfanyabiashara ndogo katika soko la Mawenzi la Mjini Morogoro.

Anasema baada ya kufariki kwa mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Mwasiti Ramadhan, ilikubalika kwamba amchukue kutoka kwa baba yake mzazi, Rashid Mvungi ambaye ana mke mwingine. Mvungi alidai kwamba ukoo ndio ulikubali mtoto alelewe na mama yake mkubwa na kwamba mkewe wa sasa hakuwa tayari kumlea mtoto huyo.

Inaelezwa kwamba mtoto huyo alikuwa akifungiwa kwenye boksi ndani ya chumba mchana mzima na wao (mama na baba mlezi) kwenda kwenye shughuli zao za kibiashara ambapo mtoto huyo hula na kujisaidia humo humo. Mtoto huyo ambaye ni mlemavu wa viungo vinavyodhaniwa kusababishwa na mazingira hayo ya kufungiwa kwenye boksi, alifichuliwa na wananchi wa mtaa huo ambao mwanzoni hakuwajua kama jirani yao anaishi na moto huyo.

Mtoto huyo alikutwa akiwa na lundo la uchafu na akiwa amedhoofu mwili kutokana na kukosa lishe bora na hewa. Baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid, anakiri kutomuona kwa muda mrefu mwanawe lakini anasema mara zote alikuwa akipeleka fedha za matumizi.

Rashid ambaye ni mfanyakazi wa Idara ya Elimu, kitengo cha Ufundi katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro anasema, “Kila nikienda kumwona nyumbani kwa mama yake mkubwa sikubahatika kumwona. Nilikuwa nikiambiwa amelala ama ametoka na watoto wenzake,” anadai.

Baadhi ya wananchi walioshughulikia tukio hilo, kwa nyakati tofauti walilaani vikali ukatili wa mwanamke huyo ambaye wakati wa tukio alinusurika kifo kwa kipigo na wananchi wenye hasira. Watuhumiwa hao walifungulia mashitaka katika kesi namba MG/ PB/5854/2014 na mara baada ya upelelezi watafikishwa mahakamani.

Katika moja ya hotuba zake za hivi karibuni, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alikemea vitendo vya wazazi na walezi wenye tabia ya kuwafanyia ukatili watoto. Waziri Simba aliwanyooshea kidole wanawake kwamba baadhi yao ndiyo wanaongoza kuwafanyia watoto vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kupindukia, tofauti na ilivyo kwa wanaume.

“Utafiti uliofanywa na wataalamu wa wizara yangu juu ya vitendo vya ukatili kwa watoto, umebaini wanawake wanaongoza kuwafanyia ukatili watoto kuliko wanaume,” alisema na kuongeza kwamba vitendo hivyo vimesababisha watoto wengi kukimbilia mitaani na wengine kugeuka kuwa ombaomba.

Maazimio ya mkutano wa kwanza wa taifa kwa viongozi waandamizi wa serikali kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto yanasema kwamba “malezi na maendeleo ya awali ya mtoto ni kigezo cha kuinuka kiuchumi na maendeleo ya jamii.”

Kwa mantiki hiyo, maazimio yanasema watoto wadogo wa umri wa miaka 0-8 wanahitaji uangalizi maalumu, matunzo na kulelewa kwa ajili ya ulinzi na makuzi yao. Huduma hizo inaelezwa huwawezesha kukua na kufikia mustakabali wenye tija na kuchangia pato la familia, jamii na hatimaye maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Watoto wadogo wanahitaji lishe bora, afya, mazingira salama, usafi, elimu ya awali, matunzo, na malezi ya kisaikolojia na msaada wenye kuwahakikishia usalama wakiwa na afya nzuri ya akili na mazingira yenye ulinzi.

zaidi ya miaka 6 iliyopita