loader
Dstv Habarileo  Mobile

Makala

Mpya Zaidi

Medali ni ndoto katika ndondi

Emmanuel MlundwaTANZANIA miaka ya nyuma ilikuwa ikifanya vizuri katika michezo mbalimbali ukiwemo wa ngumi za ridhaa, lakini miaka ilivyosonga mbele mabondia wake wamekuwa wakifanya vibaya.

Kwa miaka mingi sasa Tanzania hatujafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwa upande wa ngumi, mchezo ambao huko nyuma ulikuwa mkombozi kwa kupata medali kutoka katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Pamoja na kufanya huko vibaya, lakini viongozi wa mchezo huo nchini wa sasa na wale waliopita, wameshindwa kabisa kuunasa kabisa mchezo huo kutoka katika hali ya kuwa sawa na kichwa cha mwendawazimu.

Na hii ya kufanya vibaya katika mchezo huo wa ndondi inachangiwa na mambo kibao yakiwemo uongozi wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) kutokuwa na mpango wa kuwaendeleza vijana kwa ajili ya kuchukua nafasi za wakongwe.

Pia BFT wameshindwa kuendesha mashindano ya ndondi yenye sura ya kitaifa baada ya mikoa mingi kutokuwa na timu na badala yake mashindano yao mengi hujaza timu kutoka taasisi za kijeshi nchini kwa kuwa ndio zina mabondia wengi.

Miaka ya nyuma:

Tanzania ilivuma sana katika mchezo huo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla baada ya mabondia wake kama akina Emmanuel Mlundwa, Lucas Msomba na wengineo kuwika katika ndondi. Mbali na kutamba katika michezo kama ile ya Afrika Mashariki na hata Afrika, pia mabondia wa Tanzania waliwahi kutamba katika michezo mikubwa kama ile ya Jumuiya ya Madola.

Kikubwa zaidi Tanzania ilipata medali yake ya kwanza katika Michezo ya Jumuiya ya Madola kupitia katika mchezo wa ndondi wakati bondia Titus Simba alipotwaa medali ya fedha katika uzito wa kati.

Historia fupi:

Tanzania imeshashiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola mara 13 hadi sasa, lakini ni mabondia wachache waliowahi kutwaa medali katika michezo hiyo huku wanariadha wakiongoza kutwaa medali nyingi zaidi. Iliichukua Tanzania miaka minane kupata medali ya kwanza tangu mwaka 1962 iliposhiriki kwa mara ya kwanza michezo hiyo inayoshirikisha nchi zilizowahi kuwa koloni la Uingereza na zingine.

Awali tulianza kushiriki kama Tanganyika, lakini baada ya Muungano na Zanzibar mwaka 1964 na baada ya hapo pande hizo mbili zimekuwa zikishiriki kama nchi moja. Tanganyika ilishindwa kung’ara kwenye michezo ya kwanza iliyofanyika Perth, Australia mwaka 1962. Miaka minne baadaye (mwaka 1966) ilishiriki mashindano mjini Kingston, Jamaica na haikuambulia kitu.

Tanzania ilianza kutwaa medali kwenye ya mwaka 1970 wakati bondia Titus Simba (marehemu) alipotwaa medali ya fedha kwa kuingia fainali katika uzani wa kati na kupigwa na John Conth wa England mjini Edinburgh, Scotland.

Tanzania iliibuka tena katika Michezo ya Jumuiya ya Madola katika ndondi ilipotwaa medali kupitia kwa bondia Haji Ally Matumla aliyepata medali ya fedha katika uzito wa feather baada ya kupigwa na John Irwin wa England kwenye fainali. Bondia mwingine, Bakari Mambeya alichukua medali ya shaba kwenye uzani wa light katika michezo hiyo.

Mwaka 1994 katika michezo iliyofanyika Victoria, Canada, bondia Hassan Matumla wa Tanzania alitwaa medali ya shaba kwenye uzani wa feather na kuzidi kuliongezea sifa taifa katika michezo hiyo.

Medali ya dhahabu:

Sio tu Tanzania imewahi kutwaa medali katika michezo hiyo, pia iliwahi kutwaa medali ya dhahabu wakati Michael Yombayomba aliposhinda taji katika uzito wa bantam katika michezo iliyofanyika Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998. Hivyo tunaweza kusema kuwa, hiyo ndio medali ya mwisho kwa Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola hadi sasa na kwa takribani miaka 16 imepita tangu tulipopata medali hiyo ya mwisho.

Nini kifanyike?

BFT ina kazi kubwa ili kurejesha mchezo huo katika ramani, ambapo wanatakiwa kuwa makini na programu za kuwaendeleza vijana na bila hilo hakuna kufanya vizuri katika mchezo huo. Lakini BFT hawana kabisa programu ya vijana yenye kueleweka na badala yake mipango hiyo imekuwa mdomoni tu na hata katika makaratasi haipo kabisa.

Viongozi wa juu wa BFT kesho Jumapili wanakwenda Seoul, Korea ya Kusini kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Ndondi (AIBA) ambako wanaweza wakanufaika na mkutano huo kama hawatakuwa mabubu. Kwa sasa mabondia wengi wazuri kama akina Rashid Matumla, Nasser Mafuru, Haji Ally Matumla na wengineo umri umekwenda, hivyo BFT ilitakiwa kuanza mapema kampeni za kuwaendeleza vijana ili kuziba mapengo ya wakali hao.

zaidi ya miaka 6 iliyopita