loader
Dstv Habarileo  Mobile

Makala

Mpya Zaidi

Karanga, mihogo haiongezi lolote kwa mwanaume

Akina mama wakitembeza mihogo mibichi. Mbali na wateja wanaotaka kujiburudisha, kuna wanaoamini kwamba mihogo mibichi husaidia kuongeza nguvu za kiume lakini kisayansi hakuna ukweli.“MKE wangu amesafiri, kama angekuwepo ningenunua hizo karanga. Siku ukiona ninanunua ujue karudi,” lilikuwa jibu la mfanyakazi wa ofisi moja, akimjibu dada mmoja ambaye ana kawaida ya kutembeza karanga katika ofisi hiyo nyakati za jioni. “Lakini hizi si karanga mbichi, ni za kukaanga,” akajibu yule dada akishawishi mteja yule anunue karanga zake.

“Najua mbichi ni hatari zaidi, lakini hata hizo (za kukaanga) pia zinaweza kuniletea taabu,” akajibu yule mteja na kumfanya yule dada aende kwa mteja mwingine, ofisini ambaye alinunua karanga jioni hiyo na kujiburudisha. Kuna hii siku nyingine nilimkuta dada mmoja akitembeza mihogo mibichi kwenye beseni. Wanaume wakawa wananunua kwa wingi.

Mwanzoni nilidhani wananunua kwa ajili ya kujiburudisha lakini kumbe wana sababu. Hii ilitokana na mazungumzo haya: “Una nazi pia dada?” Aliuliza mteja moja. “Ndio, nikukatie kipande cha shilingi ngapi?” “Nikatie cha shilingi 500... Lakini nazi yenyewe imekomaa kwa sababu kama haijakomaa haisaidii kitu.” “Imekomaa vya kutosha,” akajibu yule mwanamke.

Wakati hayo yakiendelea, mwanaume mwingine aliyekuwa ameandamana na huyo anayenunua mihogo mibichi na nazi, alimwambia mwenzake kwamba yeye siku hizi ameachana na mihogo katika suala zima la kuleta “heshima ya ndoa nyumbani,” bali amehamia kwenye supu ya pweza. “Supu ya pweza?” Akahoji yule mwingine.

“Supu ya pweza ndio mambo yote. Mimi angalau kila wiki ninapata mara mbili hivi jioni na mambo yanakuwa poa,” akajibu yule mwenzake. Kwa muda mrefu, jamii imekuwa ikiamini kwamba karanga, mihogo mibichi, nazi, supu ya pweza na vingine mfano wake vinaongeza manii na hivyo kuimarisha pia nguvu za kiume.

Lakini wanaume wanaoamini hayo wakikutana na mtaalamu wa masuala ya afya uzazi, Dk Cuthbert Maendaenda ambaye pia ni meneja wa mradi wa Haki ya Afya Uzazi unaowalenga pia wanaume kama washirika sawa (TMEP) katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, watabadilisha mtazamo wao wa sasa.

Akizungumza katika semina ya wahariri iliyofanyika mjini Morogoro wiki iliyopita, Dk Maendaenda anasema mtazamo huo ni potofu kwa sababu karanga, mihogo mibichi ama supu ya pweza haviongozi lolote mintarafu suala zima la nguvu za kiume. Anafafanua kwamba vyakula hivyo sehemu kubwa vinaongeza mafuta na wanga mwilini na protini kiasi kidogo wakati mbegu za kiume hutengenezwa zaidi na protini.

“Unajua ukikamua karanga mbichi utaona kama maji yake yanafanana na manii, lakini si kwamba karanga hizo zilizokamuliwa zikiingia mwilini zitakwenda kuongeza manii moja kwa moja. Mtu akila karanga, zinaingia katika mfumo wa usagaji wa chakula na sehemu kubwa ya karanga ni mafuta kwa hiyo hazina uhusiano wa moja kwa moja na kuongeza manii. Vivyo hivyo kwa mihogo mibichi na hata pweza,” anasema.

Anatoa mfano mwingine wa matunda damu kwamba rangi haina maana kwamba ukilila linakwenda moja kwa moja kuongeza damu. “Matunda damu ni sawa na matunda mengine. Ukilila linaingia kwenye mfumo wa uyeyushaji wa chakula na ndipo kiasi kinachotakiwa na damu huchukuliwa na siyo kwamba kwa sababu ni jekundu mfano wa damu, ukilila linakwenda moja kwa moja kwenye damu,” anasema.

Anakiri kwamba kuna baadhi ya vyakula vinasaidia utengenezaji wa manii kwa mwanaume ikiwa ni pamoja na matunda, nyama, samaki na vyakula jamii ya kunde. Dk Maendaenda anasema asilimia 60 ya tatizo la nguvu za kiume kwa wanaume ni la kisaikolojia huku asilimia iliyobaki ikitokana na maradhi (kama kisukari na shinikizo la damu), matumizi ya dawa fulanifulani na umri.

“Unaweza kukutana na mtu anasema akinywa aina fulani ya bia mambo yake yanakuwa safi akikutana na mwenza wake lakini mwingine anakwambia bia fulani ndio humsaidia... Kinachofanyika hapo ni suala la kisaikolojia tu na si ile bia. Yaani bia inampa uhakika kwamba atashughulika vizuri. “Mwanaume ukishapata hisia kwamba sitaweza, sitaweza... kweli hutaweza (utapata tatizo la nguvu za kiume), lakini kisaikolojia ukiamini kwamba utaweza, utaweza, kweli utaweza,” anasema.

Anasema kwamba kwa wanaume wanywaji wa pombe, kuna kiwango ambacho kinahamasisha kufanya mapenzi na kuna kiwango kikifika mwanaume hawezi tena kurejesha heshima ya ndoa! Kuhusu dawa ya viagra, anasema ni dawa inayowasaidia wanaume wenye matatizo ya nguvu za kiume lakini pia inaleta tatizo la kisaikolojia la kuitegemea kila mara (dependency syndrome).

Wanaume kubadilika. Mradi wa TMEP unaofadhiliwa na Taasisi ya Elimu ya Ujinsia ya Sweden (RFSU) umekuwa ukitoa elimu ya Haki ya Afya ya Uzazi kwa mikoa ya Rukwa na Singida ambapo umefanikiwa kubadilisha kwa kiasi kikubwa mitazamo ya wanaume kuhusu kushirikiana na wake zao, mintarafu suala zima la afya ya uzazi.

Kwa nini wanaume? Dk Maendaenda anasema kwamba miradi mingi na hata uendaji wa kliniki wa kila mara wa wanawake umekuwa ukitoa elimu ya afya ya uzazi kwa wanawake lakini siyo kwa wanaume. Anatoa mfano kwamba hata tabia ya kubaka wakati mwingine inatokana na mila na desturi zilivyomtengeneza mwanaume na kukosa elimu mwafaka.

“Jamii inamuoa mwanamke kama mwenye nguvu, anayeweza kufanya lolote ikiwemo kumkaba mwanamke na kumwingilia bila idhini yake. Lakini mwanaume huyo akipata elimu kwamba yeye na mwanamke hawana tofauti yoyote ukiacha ya kibaolojia, akajua mengi kuhusu via vyake vya uzazi na vya mwanamke, athari za kubaka na kwamba hata mwanamke akituna anaweza akapambana naye, wale hawezi kubaka,” anasema.

Anasema Mradi wa TMEP umesaidia kuwabadilisha wanaume katika mikoa ya Singida na Rukwa ambapo wengi sasa wanashirikiana na wake zao katika uzazi wa mpango, kwenda kiliniki, na hata kusaidiana kazi za nyumbani.

Dk Maendaenda anasema mwezi Mei mwaka huu kulifanyika mkutano kuhusu Afya ya Mama na Mtoto jijini Dar es Salaam ambapo Rais Kikwete alitoa agizo kwa viongozi kwamba baada ya kuwepo mafanikio ya nyota ya kijani kwa wanawake, hatua ambayo imepunguza sana vifo vya akina mama na watoto, ni muhimu sasa elimu ya nyota ya kijani ihamie kwa wanaume.

“Nadhani Rais alizungumza vile akiwa hajui kwamba tayari kuna jitihada ambazo zinafanywa na zinaendelea. Ni vyema watoa maamuzi wajue kwamba jitihada za kuwaelimisha wanaume zipo, mifano ipo na sehemu za kwenda kujifunzia zipo. Kwamba zile halmashari katika mikoa ya Singida (Singida Vijijini, Singida Mjini, Manyoni na Ikungi) na Rukwa (Sumbawanga mjini, Vijijini, Nkasi, Matai) kuna mifano mizuri kabisa ni kwa namna gani tunaweza kuwamulikia wanaume nyota ya kijani,” anasema.

Anasisitiza kwamba ni vyema wilaya ambazo hazijafikiwa na mradi huo zikaenda kujifunza kwenye halmashauri hizo namna ambavyo wanaume wanaweza kufikishiwa elimu ya nyota ya kijani na wakabadilika. Dk Maendaenda anasema mikoa ambayo wangetamani kwenda, ingawa mradi wao uko mbioni kumalizika ni Mara na Tabora.

Anasema Mkoa wa Mara, hususan wilaya za Tarime na Serengeti kuna tatizo kubwa la mfumo dume, unyanyasaji wa kijinsia na ukeketaji ambao una athari nyingi katika haki ya afya ya uzazi wakati Mkoa wa Tabora takwimu zinaonesha kwamba una vifo vingi vya akina mama.

Tukipata rasilimali za kutosha, tutakwenda mkoa wa Mara kuona namna tunavyoweza kutumia ushiriki wa wanaume katika kukomesha ukeketaji wa watoto wa kike. “Kama tutaweza kuwabadilisha wanaume na kuwafanya wawe washiriki sawa katika masuala ya haki ya afya ya uzazi na ujinsia, nchi yetu itapiga maendeleo makubwa sana,” anasema.

zaidi ya miaka 6 iliyopita