loader
Dstv Habarileo  Mobile

Makala

Mpya Zaidi

Karate mchezo unaohitaji nidhamu

KATIKA miaka ya karibuni, mchezo wa karate au wengine wanapenda kusema mapigano, umekuwa ukihusishwa na vitendo vya uhalifu.

Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni baada ya baadhi ya watu waliodaiwa kujihusisha na ugaidi kukamatwa na baada ya uchunguzi, waligundulika wakijihusisha na mchezo wa karate.

Matukio yametokea katika mikoa ya Arusha, Mtwara na Tanga. Katika mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Karate Tanzania (TKF), Geofrey Kalonga anasema anaungana na Jeshi la Polisi Tanzania kuwa wote wanaotumia medani ya mchezo huo kufanya uhalifu wa aina yoyote wachukuliwe hatua.

Kalonga anasema miongoni mwa mambo makubwa wanayofundisha katika mchezo huo ni kuwa na nidhamu ikiwa kama sifa ya kwanza, lakini pia lengo la mchezo huo ni kumfundisha mtu kujiweka katika ulinzi salama na kuongeza ufahamu.

“Ni jambo la kusikitisha kama kuna wenzetu wanaotumia mchezo huo katika kufanya vitendo vya uhalifu, ni dhahiri kuwa wanahitaji kuchukuliwa hatua kwa wote watakaohusika,” anasema Kalonga. Anasema changamoto kubwa iliyopo ni kwamba kumekuwa na vikundi vingi mtaani vinavyojihusisha na mchezo huo, ambavyo hawavitambui na kusema hao sio wenzao.

Vikundi hivyo vimekuwa vikitengeneza mahusiano na walimu wa kigeni bila kulishirikisha shirikisho hilo, hali inayosababisha kuonekana hawafanyi kazi yao ipasavyo. Mchezo huo ambao unachezwa na zaidi ya watu milioni 25 duniani, kwa Tanzania wazazi wameanza kupata hofu baada ya kuonekana ukihusishwa na vitendo vya kihalifu.

Huko nyuma wazazi walikuwa wakionesha mwitikio kwa kuwapeleka watoto wao kujifunza mchezo huo, na sasa baadhi wanaanza kupata hofu kutokana na matukio yanayojitokeza hivi sasa. Kalonga anasema wakati wanaanzisha mchezo huo, lengo ilikuwa ni kuendeleza mchezo huo kwa kuwapatia vijana ajira.

Na wengi walijiunga na kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Hiyo ni kutokana na shirikisho hilo kujiunga na Shirikisho la Karate Duniani (WKF) ili kupata fursa ya kushiriki katika michezo ya kimataifa. Anasema mchezo huo sio tu unatumika kwa ajili ya kujiweka salama, bali pia katika makongamano ya kiheshima duniani, baadhi ya wanamichezo wamekuwa wakialikwa kushindana.

Mchezo huo licha ya kuwa Tanzania haujapewa nafasi kama ilivyo kwa michezo mingine kama vile mpira wa miguu katika nchi zilizoendelea unatambulika na kupendwa na wengi. Kalonga anasema hapa nchini bado jamii ina imani potofu kuhusu mchezo huo, wengine wakihusishwa na wizi, ujambazi, hushirikiana na mambo mengine.

“Kutokana na imani hiyo wazazi wengi hawataki kuwaleta watoto wao kujihusisha na mchezo huu, lakini ukweli ni kwamba sio kweli vitu vyote vinavyosemwa, tunashiriki,” anasema mwenyekiti huyo. Aidha, anasema wapo walimu wa mchezo huo kwa sababu ya ubinafsi wanaunda vikundi vyao pasipo kuwashirikisha na kutafuta wahisani ili wawasaidie. Hii ni changamoto kubwa kwao.

“Wapo watu wasiotaka kushirikiana nasi, wala hawatambuliki na Serikali na Baraza la Michezo, wanatangaza kuitisha mashindano ya kimataifa duniani, halafu Shirikisho letu wala Zanzibar halina taarifa yoyote, watu kama hao hatuwatambui,” anasema. Anasema licha ya kuwa mchezo huo umelenga kuwaweka pamoja, kama ubinafsi utaendelezwa miongoni mwa vikundi hawatafika mbali, kwani ushirikiano ni jambo la msingi na muhimu katika kuinua mchezo huo.

Historia ya TKF Shirikisho la Karate Tanzania limesajiliwa mwaka 2010 na kupatiwa hati ya usajili. Linaundwa na vyama viwili vinavyoshiriki katika mitindo miwili tofauti. Kuna Chama cha TAGOKA ambacho kinajihusisha na mtindo wa karate unaofahamika kama Gojuryu, na TASHOKA wanaojihusisha na mtindo unaofahamika kama Shotokani.

Mipango yao Kalonga anasema wamejipanga kuhakikisha mchezo huo unazidi kutambulika katika jamii ambapo wataenda mikoa kuelimisha. “Tumejipanga kuandaa semina ya mafunzo Tanzania bara na Visiwani, yatakayoambatana na mashindano, lengo ni kuhamasisha mchezo ili watu washiriki kama sehemu ya ajira na burudani pia,” anasema mwenyekiti huyo.

Anasema wataanza na mikoa mitano ya Mwanza, Tanga, Kigoma, Mbeya na Pemba na baada ya hapo watakuwa wanakwenda kutoka sehemu moja hadi nyingine. Lengo la kuanza na mikoa hiyo ni baada ya kugundua mchezo huo haujapewa nafasi kwa asilimia kubwa. “Tunalenga kupata vipaji, tunategemea timu yetu ya Taifa iwe na vipaji kutoka katika kona mbalimbali za nchi,” anasema.

Anasema wana mpango wa kushiriki mashindano ya Kanda ya Tano na yale ya Afrika na kama watafuzu wataenda kushiriki kwenye mashindano ya dunia na kujenga heshima ya mchezo huo. Katika kufanikisha hilo, wanakusudia kutafuta fedha kutoka kwa wadau na kampuni mbalimbali. Rai kwa wanachama Kutojihusisha na mashindano yoyote ambayo shirikisho haliyatambui.

Anasema wanaowataka lazima wawe wanatambulika wasije wakajikuta wanajihusisha katika mikono isiyo salama. Kwa mujibu wa Kalonga, TKF iko katika mchakato wa kuzungumza na serikali kuwa vikundi vinavyojiunga na watu wa kimataifa pasipo kufuata sheria za nchi au Shirikisho vidhibitiwe.

“Sisi hatuna ugomvi na mtu, tunapenda sheria zilizopo ziheshimiwe, kama watazingatia, tunawakaribisha,” anasema. Kuna umuhimu mkubwa kwa shirikisho hilo kutoa elimu kwa vikundi mbalimbali ikiwezekana kuwaonya baadhi yao wanaojaribu kuwashusha heshima kwa maendeleo ya mchezo.

Lakini pia ikiwa watakaa kimya huenda baadaye wakakosa wachezaji vijana, kwani wazazi wataendelea kupata hofu kutokana na jinsi ambavyo mchezo huo unavyohusishwa katika jamii. Vile vile, ubinafsi haujengi, zaidi hubomoa. Kuna methali isemayo umoja ni nguvu na utengano ni dhaifu.

Vikundi vote vinavyojihusisha na mchezo huo, itapendeza kama watakuwa wakishirikiana na Shirikisho lao katika kupambana na vitendo viovu, kuandaa mashindano makubwa na kuelimisha jamii kuhusu faida za mchezo huo.

zaidi ya miaka 7 iliyopita