loader
Dstv Habarileo  Mobile

Makala

Mpya Zaidi

Mtandao wa barabara waleta matumaini Rukwa

“MIMI sikutarajia kabisa kuishi nikiwa hai na kushuhudia barabara ya lami ikipita mkoani kwetu, nilijua hii inayozungumzwa ni porojo tu za kisiasa maana tangu miaka sasa tunaiona ikipita tunaambiwa hata majukwaani kuwa barabara inayounganisha Tunduma na Laela hadi Sumbawanga itajengwa kwa kiwango cha lami,” anasema Zeno Nkoswe, mmoja wa wazee maarufu mjini Sumbawanga.

“Nilihisi kuwa sisi wazee wa rika hili tutaishi na kushuhudia barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami tutakuwa tayari tumekufa,” anaendelea kusema Nkoswe. Lakini sasa stori ni tofauti kabisa kwa wazee wa rika la mzee Nkoswe ambao sasa wanashuhudia na kuona kama wako ndotoni kwani barabara hiyo sasa imejengwa si kwa kiwango tu cha lami lakini kwa ubora unaostahili.

“Kijana wangu naona kama naota kila kitu kimebadilika ule usafiri wa taabu kwenye barabara ya vumbi na tope wakati wa masika ambapo ilikuwa inatuchukua siku mbili kusafiri kwa gari kutoka hapa hadi Mbeya hususani wakati wa msimu wa masika,” anasema. “Ilikuwa ikituchukua saa zaidi ya 40 kusafiri kutoka hapa (Sumbawanga) kwenda Mpanda lakini sasa kadhia na masahibu hayo yamekuwa ni historia tu,” anasema Mzee Nkose .

Mtazamo huo wa mzee Nkoswe na wenzake wa rika lake ambao wameishi na kuona barabara kuu za Mkoa wa Rukwa sasa zikijengwa kwa kiwango cha lami unaakisi furaha ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda hivi karibuni alipowamwagia sifa kedekede makandarasi wa Kimataifa wanaojenga barabara kuu za mkoa huu inayounganisha Tunduma na Laela hadi Sumbawanga yenye umbali wa kilomita 228 kwa kiwango cha lami.

Waziri Mkuu bila kuumauma maneno anasema, “ Sasa kila kitu ni sana kwani muda wa kusafiri kutoka Mbeya hadi Sumbawanga ni mfupi sana kwa kuwa watu wanasafiri kwa vyombo vya usafiri katika barabara ya lami mwanzo hadi mwisho.” “Hawa wakandarasi wanaojenga barabara ya Tunduma – Laela Sumbawanga ambayo imekaribia kumalizika nasikia kimebakia kipande kifupi tu wanakimalizia kinachounganisha vijiji vya Kaengesa na Sumbawanga tena wanajenga kwa kiwango, hili ni jambo la kufurahisha sana,” anasema.

Waziri Mkuu Pinda anaonesha furaha yake hiyo wakati alipotembelea kambi ya makandarasi wanaojenga kipande cha barabara inayounganisha Kanazi na Kizi hadi Kibaoni kijijini alikozaliwa Waziri Mkuu Pinda kilichopo wilayani Mlele katika Mkoa jirani wa Katavi. Kambi hiyo ya ujezi iko kijijini Mpalamawe wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa.

Akiwatambulisha wakazi wa Kijiji cha Mpalamawe waliojitokeza kwa wingi kumpokea pia kumsalimia anasema kuwa licha ya kuwa yupo katika mapumziko mafupi kijijini kwake Kibaoni lakini amelazimika kutembelea kambi hiyo akiwa ameongozana na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing.

“Nimefurahishwa na kazi ya ujenzi unaofanywa na makandarasi wanaojenga barabara hizi kwa kiwango cha lami lakini bado sijaridhishwa na kazi za Kampuni hii ya ujenzi ya China Hunan Construction Engineering Group (CHCEG) kazi zake zinaenda pole pole sana.” “Sasa kwa kuwa Balozi, Dk Lu alikuwa amenitembelea pale kijijini kwangu nikamwomba tufuatane ili aje kuwaona ndugu zake kazi wanayoifanya ajionee yeye mwenyewe,” anasisitiza Pinda.

Anamwagiza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa, kuhakikisha kuwa anafuatilia kwa karibu ili kubaini sababu hasa zinazomfanya Mkandarasi (CHCEG) kutotekeleza kazi zake kwa kiwango kinachohitajika.

Kwa sasa Mkoa wa Rukwa ambao ni maarufu kwa kilimo cha mahindi na mpunga nchini ambapo licha ya wakulima kwa miaka dahali kukosa masoko ya uhakika ya kuuzia mazao yao wanazalisha mahindi mara sita ya mahitaji halisi kuna makandarasi sita wanaoboresha barabara zake kuu kwa kiwango cha lami zenye umbali wa kilomita zaidi ya 650 .

“Hii ni historia haijawahi kutokea kwani hata sasa ni Mkoa wa Rukwa nchini pekee kwa wakati mmoja ikiwa na makandarasi sita wa kimataifa wakikarabati mtandao mkubwa wa barabara kwa kiwango cha lami kwa wakati mmoja,” anasema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.

Barabara hizo ni pamoja na inayounganisha Tunduma na Laela hadi Sumbawanga mjini yenye umbali wa kilomita 228.40 ambayo ukarabati wake umegharimu Dola za Kimarekani milioni 97 kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC).

Serikali ya Tanzania akigharimikia ujenzi wa barabara kuu za mkoa kwa kiwango cha lami ikiwemo ya Sumbawanga na Namanyere hadi Mpanda /Kizi-Kibaoni yenye urefu wa kilomita 274.

Barabara hii kwa mujibu wa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Florian Kabaka katika vipande vitatu ili kuharakisha ujenzi wake kikiwemo kipande kinachounganisha Sumbawanga – Kanazi umbali wa kilomita 75 kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 78.8 na kipande cha Kanaz – Kizi - Kibaoni yenye umbali wa kilomita 76.6 kwa gharama zaidi ya Sh bilioni 82.84 na ile ya Sumbawanga-Matai- Kasanga Port yenye umbali wa kilomita 112 kwa gharama zaidi ya Sh bilioni 133.3 .

Hakika ni furaha ilioje kwa wakazi wa mkoa huu hususani wakulima kutokana na ukarabati huo mkubwa wa barabara kuu hizi kwa kiwango cha lami wakijawa na bashasha na matumani makubwa pindi ujenzi huo ukikamilika. Kwa mujibu wa wananchi wanakiri kuwa kwa sasa macho na masikio yao wameshayaelekeza kwenye masoko ya nchi jirani za Malawi, Kongo na Zambia wakiwa na matumaini makubwa kuwa bidhaa zao zikiwemo nafaka wataziuza kwa bei nzuri ya kiushindani.

“Sio siri hata kidogo barabara hizi za lami zinavutia makampuni makubwa kutoka mikoa ya jirani hata mbali kama Dar kuja kuwekeza mkoani kwetu kwani mkoa huu umejaliwa rasilimali nyingi ikiwemo ardhi na kilimo,” nasema John Siwela ambaye ni mwananchi mkoani Rukwa.

Wilayani Sumbawanga , Bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga na ufuta na kuweza kuilisha mikoa ya jirani ikiwemo Mbeya na Tabora mkulima ambaye nilikutana naye kwenye bonde hilo hivi karibuni na kujitambulisha kwangu kama Embassi Mwigulu anaeleza kuwa msimu uliopita alivuna zaidi ya gunia 1,000 za mpunga na 100 za ufuta msimu uliopita wa mavuno akiwa amejawa matumaini makubwa kuwa kukamilika kwa barabara hizo itakuwa ni faida kubwa kwao.

Licha ya ujenzi huo mkubwa wa mtandao wa barabara kuu mkoani hapa , Mhandisi Kabaka anabainisha kuwa katika jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa barabara zote mkoani hapa zinapitika wakati wote. Zaidi ya Sh bilioni 8.4 zimetumika kukarabati barabara hizo zenye umbali wa kilomita 263.7 kwa kiwango cha changarawe kupitia mradi wa Performance Based Management and Maintenance of Roads (PMMR).

zaidi ya miaka 7 iliyopita