loader

Makala

Mpya Zaidi

Mathias Mnyampala: Mtunzi aliyeacha urithi mpana wa fasihi

Charles Mnyampala, mtoto wa marehemu Mathias Mnyampala akieleza historia na maisha ya marehemu baba yake.NI Jumamosi jioni napata fursa ya kufika nyumbani kwa mtoto wa mwandishi maarufu wa fasihi andishi, Marehemu Mathias Mnyampala, aliyefariki dunia miaka 42 iliyopita na kutuachia hazina ya vitabu vyake.

Baada ya kufika nyumbani hapo na kujitambulisha, mwenyeji wangu anahoji maswali machache kisha anaingia ndani na kutoka na sanduku kubwa la chuma. Anapofika karibu na mlango anapokelewa sanduku hilo na mkewe anayelileta sebuleni, jirani na mahala nilipoketi.

“Sanduku hili lina kumbukumbu zote za marehemu baba yangu, Marehemu Mathias Mnyamapala.Huku kuna maandiko na hata picha za aina mbalimbali lakini bado naona mtunzi huyo hakumbukwi vya kutosha licha ya kutoa mchango wake katika kujenga lugha ya Kiswahili,” anasema.

Mnyampala niliyefuata habari zake hapa ni mwandishi wa vitabu vingi maarufu kikiwemo Diwani ya Lambert, Waadhi wa Ushairi, Diwani ya Mnyampala, Kisa cha Mrina Asali na Wenzake Wawili na vingine vingi. Marehemu pia aliandika historia ya maisha yake baada ya kuumwa kwa muda mrefu kuanzia mwaka 1968 hadi 1969 alipofariki dunia.

Kwa mujibu wa mwanawe, Charles Mnyampala (69) ambaye ni mtoto wa pili wa marehemu kati ya watoto watatu anasema licha ya mtunzi huyo kufanya juhudi kubwa katika kazi ya fasihi andishi huku vitabu vyake vikitumika kufundishia katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwemo vyuo vikuu, serikali haimkumbuki.

Hata hivyo, Charles ambaye ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi hakufafanua kwa kina anataka serikali imkumbuke baba yake namna gani. Akieleza chimbuko la mtunzi huyo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na kazi zake, Charles anasema marehemu baba yake alizaliwa mwaka 1917 katika kitongoji cha Mutundya, Ihumwa katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Anasema chimbuko la baba yake ni Hombolo, eneo la Chinyami Mlimani, lakini mababu na mabibi zake waliteremka milimani na kufika Ihumwa na hapo wakagawanyika, wengine wakaenda Ipagala.

“Wengine wakaenda Ipagala na wengine wakaenda Makulu kwa Mtemi Biringi na wengine wakaenda Ihumwa katika eneo hilo ndipo akazaliwa baba, mwaka 1917,” anasema na kuongeza kwamba wakati huo Mathias Mnyampala alikuwa akijulikana kwa jina la utotoni la Mzehe.

Anasema babu yake alikuwa mfua vyuma aliyetengeneza zana mbalimbali ikiwemo majembe, akapata fedha nyingi, akanunua mifugo na katika udogo wake Mathias Mnyapala alikuwa ni mchunga mifugo, ng’ombe, kondoo na mbuzi. Anasema Mnyampala aliendelea kukua na kuwa mtu mzima ambapo alianza kucheza ngoma za Nindo huku akiwa Manju (kiongozi) wa ngoma ya Kigogo ama Mwimbizi.

Alikuwa akipaka udongo mwekundu kichwani na kisha wanatia na samli katika kuimarisha utamaduni wa Kigogo, wakati huo akiendelea kuwa mtu mzima ambaye alianza kulipa kodi iliyokuwa ikitozwa na wakoloni. Charles anasema, mpaka wakati huo, baba yake alikuwa hajui kusoma wala kuandika.

Ilipofika mwaka 1925, Charles anasema familia ya Mnyampala waliondoka na makundi yao ya wanyama kuelekea Kinyambwa na ilipofika mwaka 1931, Mathias akaoa mke wake wa kwanza aliyeitwa Cecilia (sasa ni marehemu) kwa mahari ya ng’ombe 23.

Mathias kusaka elimu

Anasema ilipofika mwaka 1933 alitamani kwenda shuleni licha ya kuwa na mke na ndipo akaamua kufanya mawasiliano na mwalimu mmoja wa Bihawana lakini alipofika shuleni walishangaa kumuona akiwa na udongo kichwani kutokana na kucheza ngoma za Kigogo, mwalimu akakataa kumuandikisha shule akimuona kama mchafu.

“Baba akarudi nyumbani. Badaye akaja mwalimu wa dini kuja kufundisha watoto. Alipofika pale, baba akatamani kwenda naye. Nia yake ilikuwa kujua kusoma lakini alikataliwa kwani alikuwa ameshalipa kodi mara mbili,” anasimulia Charles. Askari Polisi huyo mstaafu anasema licha ya kukataliwa, baba yake hakukata tamaa.

Akawa anawasogelea wanafunzi waliokuwa wakisoma chini ya mti waliokuwa wakifundishwa na mwalimu aitwaye Daimon ambaye alikuwa, hata hivyo, akichukia kumuona.

“Lakini siku moja mwalimu huyo alimuita mbele ya wanafunzi na kumuambia asome. Cha ajabu baba alisoma vizuri na kuonesha kwamba ana uelewa mkubwa kuliko wanafunzi aliokuwa wakiwafundisha. “Mwalimu akampenda, akamwambia akae hapo kwani ni bora zaidi kuliko wale anaowasomesha na akaendelea kusoma na ikafika wakati akaona aongeze elimu, akamuacha mkewe na ng’ombe, jambo hilo likamuudhi baba yake.

Anasema mwaka 1934 Mathias alikwenda Bahi akiwa na Padre Aloyce Gasehys na ni huko alipopata ubatizo, akaanza kufundisha Mzogole mwaka 1936.

“Ili kujiendeleza kielimu, baadaye aliamua kwenda kuomba nafasi shule ya kati. Akaambiwa atoe ndama moja kama ada na senti 35 lakini hakuweza kumpata ndama huyo kwani mifugo alikuwa ameiacha nyumbani kwao na asingeweza kurudi kuchukua ndama kwa haraka,” anasema.

Charles anazidi kusimulia kwamba baadaye baba yake alipata wazo la kwenda kuongeza elimu maeneo ya Bigwa, Morogoro ambapo kulikuwa na shule ya sekondari lakini alipompa taarifa hizo baba yake alimtaka aondoke pamoja na mkewe la sivyo ampeleke kwao au aone ni kitu gani kingine cha kufanya. Hata hivyo, Charles anasema baba yake aliamua kuendelea na ualimu wa dini aliokuwa akifundisha.

Kazi ya ukarani

Desemba mwaka 1936 kulikuwa na nafasi ya ukarani wa kodi na alipopata habari akaandika maombi. Akaenda kupeleka maombi ya kazi akiwa amevaa lubega, tarishi mmoja akamfokea vibaya lakini baadaye alitokea tarishi mkuu aliyekuwa akitoka naye kijiji kimoja.

Baada ya kufanya usaili alifaulu akapangiwa kufanya kazi ya ukarani wa kodi na mweka hazina katika kambi ya Mirembe ambapo alifanya kazi ya ukarani kwa kipindi kirefu hadi mauti yalipomkuta Juni 8 mwaka 1969, wakati huo akiwa karani wa Mahakama Kuu.

Anasema wakati mwingi, Marehemu Mathias Mnyampala alikuwa akipeleka mashairi yake kwenye gazeti la Mamboleo. Kadhalika alikuwa akiandika habari za Ugogoni kwenye gazeti hilo na kwamba kabla ya kifo chake aliwahi kuanzisha gazeti lake likiitwa Welaa.

Miswada aliyoacha Mnyampala

“Kuna miswada mingi ya Marehemu baba, Mathias Mnyampala ambayo alikufa ikiwa bado haijachapwa. Nimejaribu kuipeleka maeneo mbalimbali wanasema hawana karatasi,” anasema.

“Alipokuwa akiumwa alikuwa akiniambia, mwanangu nimefanya kazi usiku na mchana katika uandishi huu. Usifanye uzembe watu wakanukuu kazi zangu, miswada hii iache watatokea wajukuu zangu waifanyie kazi ili vitabu vyake vitoke kama nitatangulia mbele za haki,” anasema.

Miswada saba ambayo mpaka sasa bado haijachapishwa ni Ugogo na Ardhi Yake, Mashairi ya Vidato, Mahadhi ya Kiswahili, Azimio la Arusha na Maandiko Matakatifu, Ufasaha wa Kiswahili, Hazina ya Washairi na Maisha ya Mtemi Mazengo.

Charles anasema Miswada ya baba yake iliyochapwa vitabu ni pamoja na Diwani ya Lamert, Waadhi wa Ushairi, Utenzi wa Enjili, Diwani ya Mnyampala, Ngonjera za Ukuta 1, Ngonjera za Ukuta 2, Kisa cha Mrina Asali na Wenzake Wawili, Mbinu za Ujamaa, Utenzi wa Zaburi na Historia, Mila na Desturi za Wagogo wa Tanganyika.

Vingine ni Kito cha Hekima 1, Kito cha Hekina 2, Fasili Johari ya Mashairi, Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi, Taaluma ya Ushairi na Historia ya Hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid.

Pamoja na hayo anasema mashirika yaliyokuwa yakichapisha miswada ya marehemu Mnyanpala yalisitisha kazi hiyo na matokeo yake miswada aliyoiacha haikuchapwa mpaka sasa na hata vitabu vilivyochapishwa wakati akiwa hai havijachapishwa kwa matoleo mengine na hivyo kusababisha kutopatikana kwa urahisi.

Familia yake

Anasema baba yake alikuwa na wake watatu, Cesilia aliyezaa mtoto moja, Mary aliyekuwa na mtoto moja pia na Margareth ambaye pia alibahatika kuzaa mtoto mmoja. Hata hivyo, mkewe ambaye bado yuko hai hadi sasa ni Mary. Kwa sasa. Charles anasema baba yake ana wajukuu 18 na vitukuu tisa.

Faida ya vitabu kwa familia

Charles anasema hakuna faida ambayo familia inapata kutokana na vitabu vyote vilivyotungwa na marehemu baba yake. Anasema amejaribu kuhangaika maeneo mbalimbali lakini hakuna mafanikio.

Anasema vitabu vya Diwani ya Mnyampala na Waadhi wa Ushairi vilichapishwa na Kampuni ya East Africa Literature Bureau ya Nairobi Kenya na alipofariki Mnyampala, alikuwa msimamizi wa mirathi kuhusiana na nyaraka mbalimbali.

“Kabla ya uamuzi wa shauri la mirathi tulipata taarifa kupitia Mahakama ya Mwanzo Dodoma Mjini nikapokea nyaraka zilizotumwa miaka ya nyuma,” anasema. Anasema baada ya kufungua mirathi waliletewa hundi kwa ajili ya malipo ya vitabu viwili vya Diwani ya Mnyampala na Waadhi wa Ushairi.

Anasema baada ya kufa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kampuni ya East Africa Literature Bureau ikavunjika na ndipo Tanzania ikaanzisha Tanzania Literature Bureau, Kenya wakaanzisha Kenya Literature Bureau na Uganda wakaanzisha, Uganda Literature Bureau.

Lakini baadaye Kenya Literature Bureau waliwaletea taarifa za hundi lakini hundi haikuwepo, jambo lililoonesha hundi ilikuwa imenyofolewa. Anasema wakati wa kampuni hiyo ya Kenya ikichapisha vitabu vya Marehemu Mnyampala vitabu vingine vilikuwa vikiuzwa kwenye vyuo vikuu vya nchi hiyo na vingine walikuwa wakiwauzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vikuu vingine.

“Kuna habari kwamba mpaka sasa Kenya wanauza vitabu vya Mnyampala kwa njia ya mtandao lakini familia haifaidiki na chochote,” anasema. Chales anasema mpaka kifo chake baba yake alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha wake wa ushairi na mambo mengine mengi kutokana na vitabu alivyokuwa akiandika.

Anasema kutokana pia na uzalendo mkubwa wa nchi yake Mnyampala aliwahi kupewa nishani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Ally Hassan Mwinyi mwaka 1994. Charles anasema alifanikiwa kugundua muswada mwingine wa baba yake ambao ulikuwa haujachapishwa wa ‘Maisha ni Kugharamia’ mwaka 2007 akiwa Mjini Dodoma pamoja na miswada mingine na nyaraka nyingine muhimu.

Anasema alifanikiwa kuupiga chapa muswaada huo kwa mara ya kwanza na tayari umechapwa kwa ajili ya kuwa kitabu ambacho kitazinduliwa hivi karibuni. Anasema katika kitabu hicho kuna historia ya marehemu ambayo aliiandika wakati wa uhai wake ikiwa na mtiririko wa matukio mbalimbali katika maisha yake na kwamba utatoa picha halisi ya maisha ya Mzee Mnyampala.

Aidha anasema baba yake aliandika muswada wa historia ya hayati Sheikh Kaluta Amri Abeid tangu mwakaa 1968 ikiwa ni miongoni mwa miswada ambayo baba yake aliiandika lakini haikuwahi kuchapishwa.

Anasema kutokana na hilo, mwaka 1980 alianza kufanya jitihada za kuwasiliana na mashirika ili kuhakikisha vitabu hivyo vyenye hazina kubwa ya Kiswahili na historia vinachapishwa ikiwa ni njia ya kuenzi mchango wake na wengine waliofanya kazi kubwa ya kuenzi lugha ya Kiswahili kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Anasema Desemba mwaka 2010 alifunga safari kutoka Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwatafuta watoto wa Marehemu Sheikh Kaluta Amri Abeid ili kuwaonesha muswada wa kitabu hicho. “Familia ilisoma na kuufurahia muswada huo wakaupenda na kukubali uchapishwe na sasa kitabu cha historia ya Sheikh Kaluta imetoka na kitabu hicho sasa kinauzwa,” anasema.

Watanzania Wanamuenzije Mnyampala?

Charles anasema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliwahi kufika kufanya utafiti na sasa wamefungua kanzi (database) ya Mnyampala chuoni hapo ili kutunza kumbukumbu. Pia Chuo Kikuu cha St. John wamekuwa wakitoa tuzo kwa wanafunzi wanaofanya kazi vizuri kwenye somo la Kiswahili, tuzo iliyopewa jina la Mnyampala.

Anasema mtafiti na Mhariri wa vitabu kutoka nchini Ufaransa, Mathieu Roy, Februari 2007 alifika nyumbani kwake kwa ajili ya kufanya utafiti wa maisha ya Mnyampala. “Roy nimekuwa naye kuanzia mwaka 2007 hadi 2012 na katika utafiti wake amefanikiwa kutunukiwa shahada ya Udaktari (PhD).

Itaendelea wiki ijayo ambapo mke wa marehemu atazungumza mengi zaidi kuhusiana na maisha ya Mnyampala na maisha baada ya kifo chake.

zaidi ya miaka 7 iliyopita