loader
Dstv Habarileo  Mobile

Safu

Mpya Zaidi

Acheni Dar yao na uchafu wake

SUALA la usafi katika Jiji la Dar es Salaam ni tete. Uchafu umegeuka tatizo sugu katika jiji hili ambalo ni kitovu cha mapokezi ya wageni wanaokuja nchini.

Katika maeneo mengi, uchafu umegeuka rafiki na sehemu ya maisha ya wakazi. Hawaoni aibu kuishi na kupita kwenye uchafu. Siyo ajabu kukuta chakula kikiuzwa kando ya mitaro iliyofurika uchafu au karibu na ‘madampo’ ya uchafu.

Kwenye makazi ya watu, hata wenye uwezo wa kuudhibiti , wamejisahau. Baadhi wamegeuka ‘wafugaji’ wa mbu kutokana na vichaka. Hakuna anayewajibika kufyeka licha ya kwamba sheria ndogo haziruhusu vichaka katika maeneo ya makazi.

Kwa bahati mbaya, watendaji na viongozi, wakiwemo wanasiasa, wamefumba macho yao. Wamekaa kimya wakisubiri matamasha, semina, warsha na mikutano ili wanukuliwe na vyombo vya habari wakitoa mwito, ushauri na rai kwa wananchi wafanye usafi.

Wakisharipotiwa na vyombo vya habari, huridhika kwani huwa wameshajionesha kwa wakubwa wao wa kazi kwamba wanawajibika. Hapa cha msingi, huuza sura na majina kwenye runinga na magazeti wakionesha kuchukia uchafu kwa maneno bila vitendo.

Mfano mzuri, ni pale homa ya dengue ilivyoibuka jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Yamesikika na kushuhudiwa matamko kibao kwenye vyombo vya habari. Ikaelezwa kwamba timu ya wakaguzi itapita maeneo yote kufanya ukaguzi.

Jamii ikahadharishwa kwamba nyumba itakayokutwa ikiwa na vichaka, wahusika watatozwa faini za papo kwa hapo. Zimepita siku kadhaa. Sijaona wakaguzi wala mfano wa wakaguzi kwenye maeneo niishiko. Tena nashuhudia ‘misitu’ kwenye maeneo kadhaa.

Ukweli ni kwamba, wananchi hawatishiki tena. Wameshazoea maneno matupu ya vitisho ya viongozi bila utekelezaji. Swali la kujiuliza, ni je, jiji hili limelaaniwa kwa uchafu? Mbona majiji mengine kama vile Mwanza yanang’ara kwa usafi? Je, tatizo ni wakazi wake?

Viongozi na watendaji? Ukubwa au wingi wa watu? Au je, tatizo ni siasa na utashi wa kisiasa? Mwenye majibu anaweza kunisaidia. Lakini jibu kuu ambalo naweza kujijibu ni kwamba, hakuna utashi miongoni mwa viongozi. Suala la usafi limeachwa ‘bora liende’.

Hata wenye ubunifu wa kuokoa jiji hili kutoka kwenye uchafu uliokithiri, wameamua kubaki na ubunifu wao moyoni au kwenye karatasi. Matokeo yake, wanashuhudiwa baadhi ya viongozi wakishatoka kwenye jiji hili na kuhamia kwingine, wanaonesha ubunifu wao.

Mfano mzuri ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe. Ni miongoni mwa viongozi wanaosifika kwa usimamizi wa usafi. Akiwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani humo, alibuni mkakati wa kuimarisha usafi.

Ikawa kila Alhamisi ni siku maalumu ya kufanya usafi wilayani humo. Hata alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ameendelea kusimamia mkakati huo wa usafi. Mji wa Bukoba pamoja na miji mingine mkoani Kagera inaendelea kung’ara.

Ajabu ni kwamba, Massawe huyu huyu kabla ya kupelekwa Karagwe, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Lakini haya hakuyafanya. Unadhani hakuwa na wazo hilo? Naamini alikuwa nalo.

Viongozi na hasa wabunge wa Dar es Salaam, wanayo dhamana ya kuhakikisha wanakuwa na utashi wa kunusuru hali hii. Hakuna mwingine wa kusemea Dar es Salaam yao na wananchi wake.

Kama hivi karibuni, walishupalia suala la Uda, na mmoja wao akasikika akikemea wanaotaka kuisema Dar matatizo yake, Je, uchafu siyo tatizo ambalo pia wanapaswa kupaza sauti kwa pamoja kulisemea?

Wabunge ambao ni sehemu ya madiwani, kwa nini wasipaze sauti dhidi ya halmashauri za manispaa zijipange na kuhakikisha yanakuwepo magari ya kuzoa taka kila kona ya jiji? Kwa nini wasipaze sauti, kila kona ya jiji ikawa na mapipa ya taka?

Kwa nini wasipaze sauti, watendaji wanaozembea kusimamia usafi wakawajibishwa? Utashi wa wabunge usiishie kwenye kushikia bango bungeni sakata la nani mmiliki halali wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Hii ndiyo Dar yao iliyokithiri kwa uchafu. Ni vyema wakahakikishe mshikamano unajielekeza matatizo yanayogusa wapiga kura wao moja kama hili la uchafu.

twessige@yahoo.com

zaidi ya miaka 6 iliyopita