loader
Dstv Habarileo  Mobile

Tahariri

Mpya Zaidi

Tuimarishe Muungano wetu katika miaka mingine 50 ijayo

WATANZANIA jana walikuwa katika shamrashamra za kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Miaka 50 siku kama ya jana, waasisi wa Muungano huo, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Shekhe Abeid Amaan Karume waliamua kuchanganya udongo na kuzifanya nchi hizo mbili kuwa taifa moja, ambalo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dhamira ya waasisi hao ilikuwa kuunganisha nguvu na kujenga umoja na ukaribu katika kukabiliana na unyanyasaji, ubaguzi na ukandamizaji dhidi ya weusi, ambao walifanyiwa maovu wakiwa katika nchi yao wenyewe.

Katika hotuba yake kwa Bunge la Tanganyika Aprili 25, 1964, Mwalimu Nyerere alisisitiza umuhimu wa kuunganisha nchi mbili jirani, ambazo kabla ya hapo ziliwahi kuwa nchi moja.

Katika hotuba yake hiyo, pamoja na mambo mengine alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano wa azma ya bara zima la Afrika kuwa nchi moja yenye nguvu.

Alisema: “Tunashirikiana kwa mila, kwa lugha, kwa tabia na hata kwa siasa; udugu wa vyama vya Afro Shiraz na TANU wote tunaufahamu.” Lakini wakati huo mpaka kufikia chereko za jana za Jubilei ya Dhahabu ya Muungano huo, Muungano umepitia majaribu kadhaa, hasa yenye hila za kutishia uhai wa Muungano.

Majaribu haya yanatoka katika kundi la watu wachache, wasioitakia mema Tanzania. Ni wabinafsi wanaofanya upuuzi huo kwa kujali zaidi `matumbo’ yao.

Kama alivyoeleza Rais Jakaya Kikwete juzi, wakati akipokea matembezi ya vijana na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Muungano huu ni wa kujivunia, hivyo unapaswa kuenziwa badala ya kuukandamiza.

Tunaungana na Rais Kikwete na wengine wenye nia njema na Muungano wa Tanzania, kwamba kitendo cha Muungano kudumu kwa miaka 50, kuimarika na kuendelea kustawi kwa nusu karne, hakika si jambo dogo na kamwe halistahili kubezwa, bali kupongezwa na kuigwa, kwani kuna nchi nyingi zilijaribu kufanya hivyo na kuishia kuwa vipandevipande.

Na kweli, kama nchi nyingi za ndani na nje ya Afrika, zinakuna kichwa jinsi ya kuungana na kubaki katika mshikamano, kwanini baadhi ya Watanzania wanajaribu kujitoa fahamu na kutaka kuwa kikwazo kwa Muungano huu unapigiwa mfano?

Kamwe watu wa aina hii, wasipewe nafasi ya kupanda na kusambaza mbegu mbaya, zinazoweza kuwa hatari kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Tunapenda kuwasihi Watanzania, hasa wanasiasa kuwa malumbano yanayoendelea ndani na nje ya Bunge la Maalum la Katiba, kamwe yasiwe hoja ya kutupeleka kuvunja Muungano.

Kikubwa ni kushindana kwa hoja, lakini pia kutopuuza hoja za wananchi kwa manufaa ya wachache, wenye nia ovu na Muungano huu unaopigiwa mfano.

Kwa ujumla, kila mmoja wetu awe na mchango kwa taifa katika kuulinda, kuuimarisha na kujivunia Muungano huu wa kihistoria barani Afrika ili uzidi kustawi na hata kuifikia miaka mingine 50 ukiwa na nguvu zaidi. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Muungano uweze kutimiza miaka mingine 50.

zaidi ya miaka 6 iliyopita