loader
Dstv Habarileo  Mobile

Uchumi

Mpya Zaidi

Serikali kutoa ruzuku ya bil. 4.8/- kwa sekta ya pamba

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher ChizaSERIKALI imeahidi kutoa ruzuku ya Sh bilioni 4.8 kwa sekta ndogo ya pamba ili kuwawezesha wakulima kununua mbegu bora ya pamba kwa Sh 600 kwa kilo kutoka Sh 1,200 ya awali.

Ruzuku hiyo ambayo wadau wa pamba wameipongeza kama kichocheo muhimu cha uzalishaji, ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha Tanzania inatoa pamba nyingi na bora katika msimu wa mwaka 2013-2014.

Ruzuku hiyo ilitangazwa juzi na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza wakati wa ziara yake kwenye maeneo yanayolima pamba kwa wingi katika mikoa ya Mwanza na Simiyu ambapo alidai kuwa punguzo la bei litawawezesha wakulima kuzipata mbegu hizo ambazo huzalishwa na kiwanda cha mbegu cha Quton kwa urahisi na kwa wingi.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba mkulima anazalisha pamba nyingi na bora ambayo itakuwa na bei nzuri katika soko la kimataifa,” alisema Waziri Chiza katika mikutano na wakulima wa vijiji vya Mwandu na Ngongwa vilivyopo katika katika mikoa ya Mwanza na Simiyu.

Kwa mujibu wa Waziri Chiza, Mbegu mpya na ya kisasa ina uwezo kutoa pamba kilo 1,500 hadi 2,000 endapo itapandwa kwa mfumo wa miche 22, 222 kwa kila ekari moja.

Kitendo cha serikali kutoa ahueni ya bei kwa wakulima pia ni suluhisho la mgogoro uliokuwa ukifukuta chinichini wa kupinga matumizi ya mbegu za kisasa kwa madai ni ghali.

Waziri Chiza alisema mkulima anaweza kutumia kilo sita za mbegu mpya kwa ekari moja tofauti na ile ya zamani ambapo zaidi kilo 20 huhitajika kwa ekari moja.

Tanzania ilizalisha kilo 250,000 za pamba katika msimu wa mwaka 2012- 13 ikiwa ni pungufu ya asilimia 42 ya pamba iliyozalishwa katika msimu wa mwaka 2011-12.

zaidi ya miaka 6 iliyopita