Taharuki yatanda mtoto akidaiwa kugeuka jiwe

Muonekano wa Mji wa Musoma mkoani Mara.

WANANCHI wa Mtaa wa Mgaranjabo, Kata ya Buhare, Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamekumbwa na taharuki baada ya mtoto, Amri Hamisi kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisha na kudaiwa kugeuka jiwe.

Shangazi wa marehemu, Husna Shabani alidai kuwa kifo hicho kinahusishwa na imani za kishirikina.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Halfan Haule alisema wamepokea taarifa za tukio linalosadikiwa ni la kishirikina kuwa mama mmoja ambaye anasadikiwa kuzaa watoto pacha na baada ya kujifungua familia ilimtaka apeleke watoto nyumbani kwa mwanaume na katika harakati za kuanza safari mmoja wa pacha hao alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

Advertisement

Haule alisema jiwe linalozungumzwa linadaiwa ni mtoto mwenye mwezi mmoja hivyo ameshangazwa na taarifa hizo hivyo kamati ya ulinzi na usalama inashughulikia suala hilo.

“Kwa haraka haraka tumeomba kadi ya hao watoto wawili lakini tumepata kadi moja ya huyo mtoto aliye hai na kadi ya marehemu bado haijafika, kama serikali tunaendelea kufanya mawasiliano na sehemu alikojifungulia ili kujipatia uhakika wa hao watoto wawili,” alisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgaranjabo, Deus Mluta Masanga, alisema hatua zimechukuliwa na wataalamu.

Mmoja wa wananchi katika mtaa huo, Faustine Manyama, aliiomba serikali kuiwezesha familia ya marehemu kwenda eneo alipozaliwa mtoto aliyefariki dunia ili kutambua kiini cha tatizo hilo.