Taifa Stars njia panda Afcon
H ARAKATI za timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zimegubikwa na maswali mengi baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Uganda kwa bao 1-0.
Kabla ya mchezo huo, Taifa Stars ilikuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye Kundi F, kutokana na matokeo ya mchezo wa awali dhidi ya Uganda ambao walishinda ugenini kwa bao 1-0.
Kipigo cha nyumbani dhidi ya Uganda ni kama kimevuruga hesabu za Taifa Stars, kwani kama ingeshinda mchezo huo ingehitaji pointi moja katika michezo miwili ili kuungana na Algeria kufuzu fainali hizo zilizopangwa kufanyika Ivory Coast mapema mwakani.
Mpaka sasa kwenye msimamo wa Kundi F, ukiitoa Algeria iliyopo kileleni na pointi 12, ikiwa na rekodi ya kushinda mechi zote nne vita imebaki kwa Tanzania na Uganda ambazo zinalingana kwa kila kitu kuanzia pointi, idadi ya mabao yakufunga na kufungwa.
Niger inaburuza mkia ikiwa na pointi mbili, katika vita hiyo ni kama imetolewa kutokana na ushindani wa Tanzania na Uganda lakini inaweza kufanya maajabu katika michezo yake miwili iliyosalia dhidi ya miamba hiyo kutoka Afrika Mashariki.
Kupoteza mchezo wa wiki hii kumefifisha matumaini kwa Watanzania kutokana na mwenendo wa Stars kwenye michuano hiyo ambayo mpaka sasa rekodi zinaonesha imeshiriki mara mbili tu tangu kuanzishwa kwake.
Lakini pia changamoto nyingine ni matokeo ya awali ya timu ambazo Taifa Stars inatarajiwa kumaliza nazo kwenye mechi hizo mbili dhidi ya Niger na Algeria.
Kwenye mechi za awali Stars haikupata matokeo mazuri mbele ya timu hizo, ilianza kwa kutoka sare ya 1-1 na Niger ikiwa ugenini kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Algeria kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa.
Lakini kitendo cha kulingana kwa pointi na Uganda nacho kimeongeza kufifisha matumaini kwa Stars kwani Uganda ni miongoni mwa kikwazo kikubwa na hiyo ni kutokana na rekodi ya mechi zilizopita huko nyuma ambazo Tanzania ilipoteza mbele ya Uganda.
Vita ya Tanzania na Uganda Katika Kundi F, ukiitoa Algeria ambao ndio vinara, Tanzania na Uganda ndio mmojawapo anatarajiwa kuingia hapo ili kushiriki fainali za Afcon 2023. Nikweli kwamba rekodi zinaonesha Uganda imekuwa nikikwazo kikubwa kwa Tanzania hasa katika mechi hizi za kuwania kufuzu michuano mbalimbali iwe ni Afcon au Kombe la Dunia na hata Cecafa.
Lakini kitu kizuri ni kwamba miamba hii ya Afrika imeshamalizana hivyo kazi iliyopo ni kila mmoja kupambana kivyake ili kuhakikisha mmoja wao anaungana na Algeria.
Mechi inayofuata Uganda atakuwa nyumbani dhidi ya Algeria na Taifa Stars itacheza na Niger nyumbani, mchezo huu ni lazima Tanzania kupata pointi tatu huku wakiomba Uganda ipoteze au kutoka hata sare matokeo ambayo yataifanya Stars kukaa nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi siyo herufi kama ilivyo sasa.
Kitu kizuri ni kwamba Uganda haichezi mechi zao za nyumbani kwao Uganda, inatumia viwanja vya ugenini kutokana na viwanja vyao kutokidhi vigezo vya Caf na Fifa kuchezewa mechi za kimataifa, hivyo hiyo ni fursa kwa Tanzania kushinda mechi hizo.
MIKAKATI TFF Kipigo cha Uganda kitakuwa kimelishtua hadi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wataanza mipango ya kuhakikisha timu hiyo inashinda mechi hizo mbili zilizobaki ili kufuzu fainali hizo ambazo zitafanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Moja ya mikakati hiyo nikutengeneza mazingira rafiki kwa kocha ili kupata muda mzuri wa kukaa kambini na wachezaji ili aweze kupandikiza mbinu sahihi zitakazomwezesha kupata ushindi. Kwa mechi mbili alizoiongoza Taifa Stars kocha Adel Amourch ameonekana yuko vizuri kimbinu hivyo kama kutakuwepo kwa mikakati mizuri ikiwemo kumpa kocha muda wakukaa na wachezaji kutamsaidia kupandikiza mbinu zake ambazo zitalinufaisha taifa.
Wanachotakiwa kufanya Taifa Star ili kufuzu Afcon ya Ivory Coast Ili Taifa Stars iweze kufuzu fainali hizo za Afcon, ni lazima kuwepo kwa mipango mkakati ya kushinda mechi zote mbili zilizobaki dhidi ya Niger na baadaye Algeria wakati huo ikiiombea mabaya Uganda ipate matokeo mabaya kwenye mechi zake mbili.
Katika hilo yapo mengi yakufanya kwanza kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye kikosi chake lakini pia kocha mkuu apewe muda wa kutosha wa kuwaona wachezaji ili atakapoita kikosi kwa ajili ya mechi hizo mbili zilizobaki awe na ufahamu mzuri na kila mchezaji.
Kwa matokeo ya mechi mbili zilizopita dhidi ya Uganda kocha hastahili lawama zaidi ya kupewa pongezi kutokana na kufanya kazi na wachezaji ambao nikama amechaguliwa na wakuu wa ufundi wa TFF. Kwa mapumziko mafupi ni wazi kuwa atapata muda mzuri kuwaona wachezaji kwa jicho lake na pia atapata muda mzuri wa kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya mechi hizo ambazo zitakuwa za kufa au kupona.