Takukuru Arusha yaziba mianya upotevu wa mapato

TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa mkoani Arusha (TAKUKURU) imefanikiwa kuziba mianya ya rushwa na upotevu wa mapato pamoja na kupandisha makusanyo katika mnada wa Locirwa uliopo wilayani Monduli kutoka makusanyo ya Sh milioni 3 hadi Sh milioni 6.

Hatua hiyo ni katika kuhakikisha serikali inadhibiti makusanyo ya fedha kikamilifu kutoka katika vyanzo vyake vya mapato.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa Arusha, Zawadi Ngailo amesema udhibiti huo utafanyika katika minada yote mkoani humo lengo likiwa kila mnada kukusanya mapato yanayofikia malengo au zaidi.

Ngailo alisema katika uchunguzi na uchambuzi uliofanywa ulibaini kuwa ng’ombe hulipwa ushuru wa Sh 7,500 kila mmoja, mbuzi Sh 3,000 na Sh 3,000 kwa kondoo na makusanyo ya awali yalikuwa Sh milioni 3 kwa siku katika mnada wa Locirwa.

Alisema taasisi hiyo ilipopata taarifa fiche juu ya makusanyo ya siku katika mnada huo kuwa yanaingia katika mikono ya watu wachache ilifanya uchunguzi na kubaini mambo mbalimbali ikiwemo wakusanya ushuru kuwa wachache ikilinganishwa na ukubwa wa eneo la mnada, wakusanya ushuru kukaa muda mrefu katika mnada huo na kufanya kazi kwa mazoea katika eneo hilo na fedha nyingine kupotea pasipo sababu.

Kamanda alisema baada ya uchunguzi wake, TAKUKURU ilipendekeza mambo kadhaa kwa Halmashauri ya Monduli ikiwemo ukusanyaji ushuru katika mnada huo kukusanywa na askari mgambo na baada ya mabadiliko hayo makusanyo yalipanda kutoka Sh milioni 3 kwa siku hadi milioni 6.2.

‘’Tutakuwa tukifanya hivyo katika minada yote ya kifugaji katika wilaya zote za Mkoa wa Arusha lengo ni kutaka makusanyo halisi yaweze kukusanywa na sio vinginevyo kwani Takukuru iko kwa ajili ya kuthibiti mianya ya upotevu wa mapato ‘’alisema Ngailo

Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, TAKUKURU imefanikiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 21 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 8.5 Arusha na mradi mmoja tu kukutwa na kasoro na hatua zilichukuliwa.

Kamanda awaliwaasa wahusika wa miradi kujitahidi kukithi matakwa ya utekelezaji wa miradi ili kuepuka ukiukwaji wa taratibu lengo ni kutaka kila mradi kukithi vigezo ili serikali isipate hasara.

Habari Zifananazo

Back to top button