Takukuru, Brela kushirikiana uchunguzi

WAKALA wa Usajili na Biashara (BRELA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kwa ajili ya kubadilishana taarifa za kiuchunguzi.

Katika utiaji saini huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Godfrey Nyaisa alisema matokeo hayo yametokana na kikao cha kati ya Brela na Takukuru Julai 8 na 9, mkoani Morogoro.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kubadilishana taarifa kutoka masjala ya biashara ambazo Brela ndiye mtunza kumbukumbu, kuwa na utaratibu wa kupeana taarifa.

Advertisement

“Matarajio ya makubaliano haya ni kuona uchunguzi unaenda kwa wakati na kuhakikisha Takukuru wanapata taarifa zilizo sahihi na kwa wakati huku tukianisha changamoto zilizopo katika utendaji kazi na kupendekeza kwa pamoja ufumbuzi wake,”alisema.

Nyaisa alisema mashirikiano hayo yamelenga kuhakikisha changamoto zilizopo zinakwisha na kuleta uimara na ufanisi wa taasisi hizo na kwamba watakuwa wanatoa elimu mara kwa mara kwa watumishi wa Brela juu ya masuala ya Rushwa.

Alisema hapo kabla, walianza kushirikiana ambapo kila siku Brela ilikuwa ikipokea barua sio chini ya sita kwa siku kutoka Takukuru kuhitaji taarifa za usajili wa kampuni na kupokea wito kwa ajili ya kuhitaji maofisa wa Brela kuwapa taarifa za kumbukumbu na kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kumbukumbu hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Salum Hamduni alisema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano na wadau.

Alisema mkataba huo unalenga kutia nguvu na kuimarisha ushirikiano uliokuwepo katika ya taasisi hizi mbili na wamekubaliana kushirikiana katika maeneo ya kubadilishana taarifa za kiuchunguzi kwa lengo la kupata ushahidi utakaowawezesha kufikisha watuhumiwa Mahakamani.

“Pia, tutaimarisha utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wa Brela kuhusu madhara ya rushwa na namna watumishi wa taasisi hizi mbili waweze kushiriki katika mapambano, kushirikiana kufanya utafiti na mifumo ili kubaini na kuziba mianya ya rushwa.”alisema.

Alisema mahusiano hayo yatakwenda kuimarisha zaidi mashirikiano yaliyokuwepo, yatarahisisha na kuharakisha utendaji wa kazi zao.

13 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *