Takukuru Iringa yaokoa Sh milioni 68
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Iringa imeokoa zaidi ya Sh milioni 68 zilizokuwa zipigwe na kuingizwa katika mifuko ya watumishi wasio waadilifu katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Akitoa taarifa ya robo ya Aprili hadi Juni 2023, Kaimu Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Bahati Haule alisema ujanja uliotaka kutumika kuiba fedha hizo umebainika baada ya taasisi yao kufuatilia matumizi ya halmashauri hiyo katika kipindi hicho.
Alisema fedha hizo zinajumuisha zaidi ya Sh milioni 30 iliyookolewa kwenye ununuzi wa bati 2,402 kwa ajili ya shule za msingi 10 zilizokuwa zinunuliwe kwa Sh 48,000 kwa kila bati badala ya Sh 35,000.
“Aidha katika uchambuzi wa mifumo, Takukuru ilibaini katika kipindi cha miezi 10 vibarua zaidi ya 46 wa halmashauri hiyo walikatwa zaidi ya Sh milioni 30.6 kutoka katika mishahara yao kwa ajili ya kuwasilishwa katika mfuko wa hifadhi wa jamii lakini hazikuwasilishwa.” alisema.
Baada ya ufuatiliaji huo, alisema ofisi yao ilipokea barua kutoka halmashauri hiyo ikieleza kwamba fedha za michango wa vibarua hao zimelipwa kwenye akaunti ya PSSF tawi la Iringa.
Aidha alisema Takukuru ilifuatilia ujenzi wa Hospitali ya Mji Mafinga na kubaini kwamba katika ujenzi huo kulifanyika malipo ya mabati 80 ya zaidi ya Sh milioni 7.7 ambayo hayakufika katika eneo la ujenzi lakini baada ya ufuatiliaji huo kufanywa fedha hizo zilirejeshwa.
“Bila ufuatiliaji huu, kiasi hicho ambacho jumla yake ni Sh milioni 68.4 kingeingia mifukoni mwa watumishi wasio waadilifu.
Nitumie fursa hii kuwaonya watumishi wote kwamba Takukuru haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria yoyote atakayethubutu kufanya ubadhirifu wa fedha na rasilimali za umma,” alisema.
Alisema katika robo hiyo, Takukuru imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 14 yenye thamani ya Sh bilioni 13.
8 katika sekta za afya elimu, barabara, masoko na ujenzi na kati yake miradi minne ilionekana kuwa na mapungufu na hatua mbalimbali zimechukuliwa.
“Takukuru Mkoa wa Iringa inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za kufichua vitendo vya rushwa na wala rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha wahusika kuchukuliwa hatua,” alisema.