TAKUKURU kuchunguza tuhuma madaktari Manyoni

Baadhi ya wanancji wa Manyoni waliohudhuria mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

BAADHI ya madaktari kwenye Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida wamelalamikiwa kuingia kazini huku wakiwa wamelewa na kushindwa kuhudumia wagonjwa, hususan wanaofika nyakati za usiku.

Malalamiko hayo yalitolewa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, ambao ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa huo Singida, Peter Serukamba, ili kusikiliza na kupatia ufumbuzi kero zinazowakabili

Mwananchi Prisca Maleta amesema Januari 4 mwaka huu, alimpeleka mtoto wake aliyekatika kidole, walifika kwenye hospitali hiyo saa tatu usiku na kukaa mpaka saa saba usiku bila kuhudumiwa.

Advertisement

Badala yake aliambiwa kama anaishi jirani, wapewe vyombo vilivyotakiwa kutumiwa kumuhudumia mgonjwa wakavichemshe kwa sababu vilikuwa vichafu.

Huku akiungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo, Maleta ameomba wasaidiwe kuondolewa kero hizo kwa sababu wananchi wengi wanaathiriwa na hali hiyo.

Serukamba ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo, kuchunguza utendaji wa watumishi, wakiwemo madakatari katika hospitali hiyo na apelekewe taarifa ya uchunguzi huo Ijumaa, wiki ijayo.

Amesema utaratibu huo wa kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzipatia utatuzi papo hapo ni endelevu na kwamba atakutana na wananchi katika kila wilaya mara moja kwa mwezi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wananchi kwenye mkutano huo(Picha zote na Editha Majura).

Licha ya hayo, malalamiko yaliyotawala mkutano huo ni migogoro ya ardhi, ambapo uamuzi ulifikiwa kwamba kamishna wa ardhi wa mkoa ashirikiane na watumishi wa ardhi wa wilaya hiyo kupitia migogoro yote ya viwanja na watoe mapendekezo kuhusu njia zinazoweza kuimaliza zikiwamo za maridhiano.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Fadhili Chimsala. aliagizwa kushirikiana na watendaji wake kuorodhesha migogoro yote ya umiliki wa mashamba na usafishaji wake, waite kila muhusika na kuzungumza naye kinagaubaga mpaka wafikie maafikiano, yaandikwe na kutiwa saini na pande zote husika.

Wakati Kamishna wa Ardhi amepewa muda wa miezi miwili itakaokoma Machi 30 Mwaka huu kuwa amekamilisha kazi hiyo, Mkurugenzi ametakiwa ifikapo Februari 20 mwaka huu awe amekamilisha kazi hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *