TAKUKURU kufuatilia rushwa kwenye tumbaku
MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Tushwa (TAKUKURU) mkoani humo ndani ya siku 28 kufanya uchunguzi wa kina, ili kuweza kubaini watu au mtu aliyepewa hongo ya aina yoyote, ili aweze kuvuruga kilimo cha tumbaku na masoko yake.
Ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa msimu wa masoko ya tumbaku 2023/2024 uliofanyika katika Chama Cha msingi Nsimbo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani humo, mara baada ya kupokea baadhi ya changamoto kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya Mkwawa Leaf ya kuwepo kwa baadhi ya watu wachache wanaovuruga utaratibu uliowekwa na serikali wa kusimamia suala la upatikanaji wa mnunuzi.
“Hapa imetajwa habari ya hongo na watu kupewa pikipiki na habari za watu kusaini mikataba usiku, sasa sisi serikali tuko hapa kwa ajili ya kusimamia maslahi ya wakulima wetu, na hatutakubali rushwa itumike kwa ajili ya kufanya jambo lolote lile nje ya maslahi ya mkulima,” amesema.
Hata hivyo amewaagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi pamoja na Kamanda wa TAKUKURU mkoa huo kuanza ufuatiliaji usiku na mchana, endapo watabaini mtu au watu wanafanya utoroshaji wa tumbaku kuwachukulia hatua kali ikiwa ni pamoja na kuitaifisha tumbaku yenyewe.
“Tafadhalini sana msijiingize kwenye biashara ya magendo ya kwenda kutorosha tumbaku na kuzipeleka kusikojulikana, utaratibu mzuri umewekwa wa zao la tumbaku kuuzwa kwenye vyama vya msingi ambako ndiko umekopeshwa pembejeo,” amesema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo mmiliki wa Kampuni ya Tumbaku ya Mkwawa Leaf , Ahmed Huwel ameiomba serikali ya Mkoa huo kuwaruhusu wakulima kufanya maamuzi ya mwekezaji wanayemtaka, huku akidai kuwa kumekuwa suala watu kukaa chini ya miti ya miembe usiku wa manane kusaini mikataba bila kuwashirikisha wakulima.
“Kama wakulima hawa wataona Mkwawa anawafaa,basi waendelee kuwa na Mkwawa, na kama wataona hawamfai wana haki ya kumfukuza na kumtafuta mtu mwingine, tunaomba sana utumie nguvu kujaribu kuwaelimisha watu wa ushirika kwamba sauti ya mkulima inahitaji kusikilizwa,” amesema Huwel.
Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la Wakurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Said Ntahondi ameishukuru serikali kwa kuileta Kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco L.
t.d, huku akisema kuwa kwa msimu uliopita Tanzania ilizalisha kilo zisizopungua milioni 60 katika zao la tumbaku.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya zao la Tumbaku mkoani Katavi Meneja Bodi ya Tumbaku Mkoa huo, Genwin Swai amesema Mkoa wa Katavi kwa msimu uliopita walitarajia kuzalisha tumbaku zaidi ya kilo milioni 15 zilizotarajiwa kuzalishwa kwenye hekta 11,092.
Amesema miongoni changamoto ambazo zilizo ukumba msimu uliopita wa kilimo cha tumbaku ni kutofikiwa kwa malengo ya uzalishaji, baadhi ya wakulima kuendelea kuchanganya tumbaku, ambapo tumbaku yenye ubora wa juu inachanganywa na yenye ubora wa chini ili kumdaganya mnunuzi, pamoja na baadhi ya wakulima kushindwa kurejesha madeni ya mikopo ya pembejeo za kilimo cha tumbaku.