TAKUKURU wambeba aliyekana sahihi yake, madeni CHAMWAI

MWENYEKITI wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu Iramba (CHAMWAI), Ali Mwekwa, amekana kutia saini nyaraka tofauti ambazo zinathibitisha kuwa alikopa zaidi ya Sh Mil. 38 kwenye Chama hicho, kwa nyakati na miaka tofauti akiwa kwenye wadhifa huo.

Imeelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, ambaye kwa sasa amehamishiwa wilayani Monduli kuwa kutokana na deni hilo kutolipwa kwa wakati na kwa ukamilifu, sasa  linazidi Sh Milioni 94.

Licha ya nyaraka tofauti ikiwemo barua ambayo Mwekwa aliiandika miaka ya iliyopita akikiri kudaiwa Sh Mil. 94 kuwasilishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amesema aliandika barua hiyo kwa kulazimishwa na polisi.

Serukamba aliyekutana na walimu wastaafu zaidi ya 100 kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisini kwake, akaita waliokuwa viongozi wenzake ili wasaidie kubaini ikiwa sahihi hizo ni za mwenzao au la na wote wakasema ni sahihi za Mwekwa ambaye hata hivyo, ameshikilia msimamo wa kuzikana.

“Viongozi wenzangu wa TAKUKURU na polisi, ninaomba muondoke na huyu mzee, mtumie wataalamu wa miandiko kuchunguza ikithibitika ni sahihi na muandiko wake, tumshitaki kwa jinai,” Serukamba akaagiza.

 

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CHAMWAI, Mwl. Mstaafu Ali Mwekwa (aliyesimama) akijieleza kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mzalendo Madege, akamkabidhi kwa polisi, wakaondoka naye.

Januari 25 Mwaka huu,  Serukamba alikutana kwa mara ya kwanza na walimu hao wakiomba awasaidie kulipwa stahiki zao wanazozidai CHAMWAI, ambacho hata hivyo kimekufa kutokana na baadhi ya wanachama wakiwemo waliokuwa viongozi wake, kutolipa fedha walizokuwa wakikopeshwa.

Baada ya majadiliano na kupitia baadhi ya vielelezo, alimuagiza DC Mwenda kukamata na kuweka mahabusu waliokuwa viongozi wa chama hicho na kuwafikisha kwenye mkutano ambao ulikusudiwa kufanyika Januari 31.

Aidha ilielezwa kuwa kila mwanachama alikuwa akikatwa Sh 10,000 kila mwezi, ambazo zilitakiwa kuingizwa kwenye akaunti ya CHAMWAI katika Benki ya CRDB, lakini baadhi ya fedha zikawa zinaishia mikononi mwa halmashauri za Iramba na Mkarama.

Hata fedha zilizoingizwa kwenye akaunti hiyo ya CRDB, hazikufika kwa chama kwa maelezo kwamba kulikuwa na mikopo iliyochukuliwa, hivyo kila shilingi iliyopokewa na CRDB ilichukuliwa kulipa deni, ambalo wanachama walimueleza Serukamba kwamba hawakuidhinisha mikopo husika.

 

MWEKAHAZINA wa CHAMWAI, Amos Mgitu akizungumza mbele ya RC Serukamba

Serukamba ameagiza Meneja CRDB kuhakikisha anapeleka nyaraka zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za kutoa mkopo kwa chama cha ushirika, ikiwemo muhtasari, ambao umetiwa saini na robo ya wanachama, kuridhia mkopo husika vinginevyo, benki itatakiwa kurudisha fedha ilizochukua kwa madai ya kujilipa deni.

Pia wakurugenzi wa halmashauri za Iramba na Mkalama wametakiwa kulipa fedha wanazodaiwa na CHAMWAI haraka na kwa ukamilifu, ili kifufuke na kiweze kulipa walimu wanaokidai.

Pamoja na Mwekwa, viongozi wengine waliosomewa madeni yao ni pamoja na Samwel Sima anayedaiwa zaidi ya Sh Milioni 9, huku Jackson Marumi mwenye deni la Sh Mil. 34.555 ikielezwa na DC Mwenda kuwa licha ya kwamba alikiri kwa maandishi kudaiwa, alifariki na halmashauri haikulipa deni hilo mpaka familia ikafunga mirathi.

Halmashauri zimeelekezwa na Serukamba kulipa fedha zote ambazo hazikulipwa kwa chama hicho na watumishi kutokana na uzembe uliofanywa na wakurugenzi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x