TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania ( TAKUKURU), Mkoa wa Morogoro imeanza kazi ya kufuatilia kwa karibu fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na mabweni ya wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza mwaka 2023 mkoani humo.
Ufuatiliaji huo wa karibu unalenga kujiridhisha na kuona iwapo fedha hizo zimetumika kwa lengo lililokusudiwa na ujenzi wake imezingatia viwango vya ubora.
Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Manyama Tungaraza amesema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa kipindi cha Julai mwaka huu hadi Septemba , 2022.
” Niwakumbushe wasimamizi wa miradi hiyo waweze kutekeleza kwa haraka kama maagizo yaliyotolewa ifikapo mwezi Januari 2023 , wanafunzi wa kidato cha kwanza waweze kuanza masomo yao “ amesema Tungaraza
Pia amesema Takukuru inaendelea kufualilia matumizi ya mbolea ya ruzuku zilizotolewa na serikali kwa ajili ya wakulima mkoani humo.
Tungaraza ametoa rai kwa wote watakaojihusisha na udanganyifu wowote kwa ajili ya kuhujumu mbolea ya ruzuku , watachukuliwa hatua kali.
Amesema kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2022, Takukuru imeweka mikakati ya kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika miradi inayotekelezwa mkoani humo kwa kushiriana na taasisi zilizopewa jukumu la kuteleleza miradi hiyo.
Amezitaja baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) , Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) na halmashauri za wilaya zilizilizopo mkoani huo.
Takukuru imefanya mawasiliano na Meneja wa TARURA na RUWASA ambao wameafiki kufanya ukaguzi wa miradi kwa kushirikiana na kwamba mawasiliano yatafanyika kwa taasisi zilizobaki kwa maana ya Tanroads , Moruwasa na halmashauri za wilaya za mkoa huu” amesema Tungaraza.
Amesema jukumu lingine ni kufuatilia kwa ukaribu mifumo ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma na kuendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa jamii kupitia mpango wa Takukuru inayotembea , pamoja na mikutano ya hadhara .
Takukuru pia inaendelea na uchunguzi wa miradi mitatu ya sekta ya afya ambao uko katika hatua mbalimbali inayohusu miradi hiyo ambayo ilikataliwa kuwekewa mawe ya msingi na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 kwa maelekezo kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge ya kufanya uchunguzi ili kubaini thamani halisi ya fedha za miradi hiyo.
Miradi hiyo ni ujenzi wa kituo cha Afya Itete wilaya ya Malinyi wenye thamani ya Sh milioni 345.2 , mradi wa kituo cha afya Igima wilaya ya Kilombero wenye thamani ya Sh milioni 500 na mradi wa jengo la wagonjwa wa dharura Hospitali ya wilaya ya Gairo wenye thamani ya Sh milioni 300 .