Takukuru yabaini madudu ujenzi wa shule Geita

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita imebaini uwepo wa viashiria vya ubadhilifu na ufujaji wa pesa katika miradi ya ujenzi wa shule tatu zenye jumla ya Sh bilioni 1.

47.

Miradi hiyo ni shule ya sekondari Nyantorotoro yenye thamani ya Sh milioni 584.2, shule ya msingi Nyantorotoro iliyogharimu Sh milioni 181.6 na shule ya msingi Museveni iliyogharimu Sh milioni 705.

Advertisement

Naibu Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita, Azza Mtaita amebainisha hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Geita na kueleza tayari uchunguzi unaendelea kwa hatua za kisheria.

“Katika uchunguzi kuna wale watu wamehojiwa, kuna wengine hawajahojiwa, lakini tutatambue tu kwamba tumeanzisha uchunguzi.” Amesema Mtaita.

Mtaita ameeleza uchunguzi wa awali unaonyesha katika miradi ya ujenzi wa shule ya msingi na shule ya sekondari Nyantorotoro makosa makubwa ni ukiukwaji wa taratibu za maununuzi.

“Hii inapelekea baadhi ya vitendea kazi au malighafi za ujenzi kununuliwa kwa bei ya juu bila kufuata taratibu za ushindanishi.

” Amesisitiza na kuongeza;

“Wakati mwingine inapelekea miradi kutokukamilika kwa wakati, sasa ni nani anachunguzwa, hilo tuachieni wakati ukifika tutatoa majibu.”

Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyantorotoro, Mwalimu Mbusiro Marwa amesema ujenzi ulianza rasmi Julai 31, 2023 na taratibu zilifuatwa kuwapata mafundi 10 kwa ajili ya ujenzi.

Amesema mradi huo ulihusisha ujenzi wa jengo la utawala, vyumba vinane vya madarasa, ofisi mbili za walimu, majengo matatu ya maabara, jengo la Tehama, jengo la maktaba, matundu nane ya vyoo.

Mbusiro ameeleza mpaka sasa kiasi cha sh milioni 566.4 zimekwishatumika, na kiusalia na kiasi cha sh milioni 17.8 kwa ajili ya malipo ya milango 15 iliyobaki pamoja na mafundi ujenzi.

Amesema mpaka sasa hakuna pesa kwa ajili ya uwekaji sakafu kwenye baadhi ya majengo, uunganishaji wa mifumo ya umeme na maji pamoja na ununuzi wa samani za ofisi na maabara.