Takukuru yagusa miradi 5 Wilaya Tanganyika
TAKUKURU Mkoa wa Katavi imebaini mapungufu mbalimbali ikiwemo usimamizi mbovu kwenye ujenzi, ukiukwaji wa mikataba na ucheleweshwaji katika kukamilisha miradi mitano ya maendeleo iliyopo Halmashuri ya Wilaya ya Tanganyika yenye thamani ya Sh milioni 661.
Akitoa taarifa ya kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2023 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Faustine Maijo amebainisha miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa bweni la shule ya msingi Kakoso kwa thamani ya Sh milioni 100, ujenzi wa maabara ya shule ya msingi Kakoso kwa thamani ya Sh milioni 300.
Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa nyumba za walimu Shule ya Msingi Lwega kwa thamani ya Sh milioni 97, ujenzi wa ofisi ya Kijiji cha Lwega kwa thamani ya Sh milioni 64 na ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Karema kwa thamani ya Sh milioni 100.
Amesema katika uchunguzi wao walibaini usimamizi mbovu, ucheleweshwaji, ukiukwaji wa taratibu za mikataba kwa kujengwa kinyume na viwango vilivyobainishwa kweye mikataba, thamani ya miradi kutoendana na fedha iliyotolewa kutekeleza mradi, pamoja na ucheleweshwaji unaotokana na ukosefu wa fedha za kutekeleza miradi.
Amesema baada ya uchunguzi huo wamechukua hatua mahsusi za kuwashauri wahusika kuhakikisha ujenzi unakamilishwa kwa wakati na kwa usimamizi madhubuti, kufuata na kurekebisha maeneo ambayo hayakufuata mkataba, wameanzisha uchunguzi pamoja na ufuatiliaji wa kuhakikisha fedha zinapatikana ili kukamilisha miradi inayoendelea.