Takukuru yaokoa bil 14/-, mali za bil 2/- zataifishwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imeokoa zaidi ya Sh bilioni 14 katika oparesheni za uchunguzi na ufuatiliaji.

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Salum Hamduni amesema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana alipokuwa akiwasilisha taarifa ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu, Dar es Salaam jana.

Hamduni alisema kupitia oparesheni, Sh bilioni 14.4 na dola za Marekani 14,571 ziliokolewa kutokana na ukwepaji kodi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.

“Kati ya hizo fedha Sh bilioni 8.4 ziliokolewa kutokana na ukwepaji kodi, bilioni 2.6 zilirejeshwa katika miradi ya maendeleo iliyokusudiwa pamoja na fedha za wananchi waliodhulumiwa na vyama vya msingi katika mikoa ya Manyara, Rukwa, Katavi, Kigoma, Morogoro, Mtwara, Simiyu, Pwani, Songwe na Mwanza,” alisema.

Hamduni alisema pia Takukuru ilifanya uchunguzi na kukamilisha majalada 1,188, majalada 16 kati ya hayo yanayohusisha kesi kubwa za rushwa zinazohusu ikiwamo ubadhirifu katika kampuni ya mabasi yaendayo haraka (UDART) yenye thamani ya Sh bilioni 8 na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Sh bilioni tatu.

Alisema majalada mengine 100 yalikamilika kutokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) yakiwamo manane yaliyohusu ubadhirifu wa fedha za Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19.

Alitaja majalada mengine yalikuwa 34 yaliyohusu kesi ya ushirika na wanachama wa chama cha ushirika wa kilimo na masoko (AMCOS) Mkoa wa Simiyu na majalada 23 kati ya 37 yenye thamani ya Sh bilioni 13.97 yaliyohusu uchunguzi wa miradi iliyotuhumiwa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kuwa na vitendo au viashiria vya rushwa.

Alisema majalada 201 yaliyohusu uchunguzi wa vitendo vya rushwa katika ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri yalikamilishwa na kuchukuliwa hatua. Hamduni alisema katika majalada hayo kesi 468 ziliamuliwa mahakamani na kutolewa hukumu, mashauri 262 sawa na asilimia 60.26 watuhumiwa walikutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo na kulipa faini na kesi 186 sawa na asilimia 39.74 watuhumiwa waliachiwa huru.

Alisema Takukuru kwa kushirikiana na ofisi ya mashtaka ya taifa ilifungua kesi mpya 646 katika mahakama nchini zikiwemo kesi 10 za rushwa kubwa zilizofunguliwa katika Makahama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi).

Hamduni alisema pia walitaifisha mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.05. Aidha, alisema Takukuru inaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia ya kutaka wazuie rushwa kabla haijatokea na katika kufanya hivyo uchunguzi ulibaini kuwepo kwa kasoro katika utekelezaji wa mkataba wa ununuzi wa umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya Pan African Energy Petroleum Tanzania (PAET).

“Tulizuia hasara ya dola za Marekani bilioni 81.99 ambayo serikali ingepata kutokana na tanesco kutozingatia masharti ya mkataba,” alisema Hamduni. Baada ya Takukuru kubaini hasara hiyo iliwaita Tanesco na PAET kwa nyakati tofauti na kupitia majadiliano PAET walikubali kuwapa Tanesco haki ya kutumia gesi ya dola milioni 40.73

Habari Zifananazo

Back to top button