Takukuru yaonya ubadhilifu pembejeo

Yarejesha mamilioni ya fedha.

TAASISI  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imeanza ufuatiliaji wa  zoezi la ugawaji pembejeo za kilimo zenye ruzuku ili kuzuia vitendo vya ubadhilifu.

Mkuu wa Takukuru Dodoma, Sosthenes Kibwengo, akizungumza leo Novemba 29, amesema wameamua kufuatilia ili kuhakikisha lengo la Serikali linatimia.

Kibwengo amewataka watakaohusika na mchakato wa ugawaji wa pembejeo hizo kuzingatia taratibu kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaohusika na ufujaji.

“Huko nyuma kulikuwa na udanganyifu katika zoezi la ugawaji wa pembejeo za kilimo zilizokuwa na ruzuku hadi kusababisha kufunguliwa mashauri ya jinai mahakamani dhidi ya baadhi ya watendaji na mawakala wa pembejeo za kilimo, tumeanzisha ufuatiliaji kwa mwaka huu ili kuhakikisha lengo la serikali linatimia.” Amesema Kibwengo

Aidha, Kibwengo amebainisha hatua mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo katika kudhibiti vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma.

Amesema katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu wamefanikiwa kurejesha shilingi milioni 75.5 zilizokuwa mikononi mwa mawakala wanaotumia mashine za kielekroniki kukusanya mapato na kuziwasilisha benki.

Amesema wanaendelea kushirikiana na halmashauri za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha ushuru na tozo zinazokusanywa kwa njia ya mashine zinawasilishwa benki kwa wakati.

”Tumefuatilia miradi 31 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 19.98 katika sekta za umwagiliaji, maji, afya, elimu na ujenzi  ambapo mapungufu yamebainishwa  yalirekebishwa  na shilingi milioni 266.5 ambazo zililipwa bila kazi zinafuatiliwa.

Aidha Kibwengo ameeleza mikakati ya TAKUKURU katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu ni kuelimisha wananchi ili kuhamasisha ushiriki wao katika kuzuia rushwa kwa kuongeza vipindi vya uelimishaji kwa njia ya redio.

Ametaja mkakati mwingine kuwa ni kuchochea uitishaji wa wananchi kwenye mikutano ya kisheria ya mitaa,vijiji na kuelimisha wananchi katika mikusanyiko mbalimbali hasa maeneo ya pembezoni.

Habari Zifananazo

Back to top button