TAKUKURU yawakalia kooni ardhi Temeke
DAR ES SALAAM: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, imebaini kuwapo madudu katika Idara ya Ardhi Manispaa ya Temeke.
Pia imewasimamisha kazi maofisa wawili wa Halmashauri ya Kigamboni kutokaa na uzembe za ujenzi wa shule mbili za Sekondari zilizogharimu Sh milioni 700.
Akizungumza leo Aprili 24, 2024, Kaimu Naibu Mkuu wa TAKUKURU Temeke, Ismail Bukuku, amesema ufuatiliaji walioufanya kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia Januari hadi hadi Machi mwaka huu walibaini sekta ya ardhi inaongoza kwa urasimu.
Amesema kwa kipindi hicho TAKUKURU imebaini kuwepo kwa urasimu katika utoaji hatimiliki na vibali vya ujenzi, na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi katika halmashauri hiyo.
“Maafisa ardhi Manispaa ya Temeke, wamekuwa wakilalamikiwa kuwa na urasimu mwingi wa utoaji hatimiliki na vibali vya ujenzi,” amesema Bukuku.
Akitoa takwimu za malalamiko yaliyohusu vitendo vya rushwa, Bukuku amesema katika kipindi hicho cha robo mwaka wamepokea malalamiko 54 huku sekta ya ardhi ikiongoza kwa malalamiko 12, ikifuatiwa na binafsi malalamiko tisa na sekta elimu ikiwa na malalamiko saba.
Rushwa kwa upande makatibu kata imeripotiwa malamamiko manne, sekta ya beanki manne, Polisi matatu, NEMC, TARURA, ujenzi, TASAF, mahakama, michezo, TRA, uhasibu, ustawi wa jamii na biashara kila moja imeripotiwa lalamiko moja wakati sekta ya utawala malamiko ya rushwa yaliyoripotiwa ni mawili.
Bukuku amesema, malalamiko waliyopokea yasiyohusu rushwa ni tisa yakihusisha sekta ya ardhi matatu, binafsi, elimu ya msingi, polisi, uhamiaji, afya na ustawi wa jamii kila moja likiwa na lalamiko moja.
Amesema TAKUKURU imewasimamisha kazi maofisa wawili wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ili kupisha uchunguzi kutokana na uzembe wa ucheleweshaji wa ujenzi wa shule mbili za Sekondari zilizopo Kigamboni.
“TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi miwili inayotekelezwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, miradi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 700, ilihusu ujenzi wa shule ya Sekondari Vumilia Ukooni ambayo ilitengewa Sh milioni 350 na shule ya Sekondari ya Mbutu ambayo nayo ilitengewa Sh milioni 350,”amesema Bukuku.
Isome pia: https://habarileo.co.tz/samia-tutafanyia-kazi-ripoti-ya-cag-takukuru/
Amesema, baada ya ufuatialiaji TAKUKURU ilibaini uzembe wa baadhi ya watumishi ambao walisababisha ucheleweshwaji wa mirad hiyo kinyume na maelekezo ya Katibu Mkuu TAMISEMI.
“Baada ya kuwasilisha matokeo ya ufuatiliaji kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo, watumishi waliohusika na uzembe wamechukuliwa hatua ya kusimamishwa. Hata hivyo, TAKUKURU itapita tena kwenye miradi hiyo ili kuona namna ushauri huo ulivyotekelezwa,”amesema Bukuku.
Watumishi wa Manispaa ya Kigamboni waliosimamishwa ni Restituta Mtaita aliyekuwa Mkuu wa Divesheni Elimu Sekondari na Joseph Mhere aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi.
Wakati huohuo, Bukuku amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke imefanikiwa kudhibiti ujenzi wa maghala (Godowns) uliokuwa unafanyika tofauti na kibali cha ujenzi kilichotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.
Bukuku amesema, kibali kilichotoka ni wa ujenzi wa ghala moja eneo la Buza kwa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, lakini ujenzi uliofanywa na kanisa hilo ni maghala matatu. Vipimo vya maghala hayo havikulingana na vipimo viliyotolewa na Mkurugenzi huyo.
“Kutokana na hali hiyo, kanisa hilo limetoa faini ya Sh million 14,”amesema Bukuku.