Tamasha la utalii wa kiutamaduni laiva Bariadi

SIMIYU: Mkuu wa Wilaya ya Bariadi,  Simon Simalenga ameipongeza kampuni ya Kilimanjaro one Travel and Tours kwa kuunga mkono kwa vitendo juhudi za serikali katika kukuza utalii wa kiutamaduni.

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo ofisini kwake wakati akifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa kampuni ya Kilimanjaro One waliotembelea ofisini kwake kufanya mazungumzo kuhusu tamasha la Lake Zone Cultural and Tourism Festival ambalo litafanyika Bariadi Simiyu July 5, 6 na kilele chake ni July 7, 2024.

“Tamasha hili linaendana na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila halmashauri inaandaa tamasha la utamaduni na utalii,” amesema.

Simalenga amesema serikali iko tayari kutoa ushirikiano kwa waandaaji hao na kuwakumbusha kuwa wasukuma wanathamnini utamaduni wao na huwa wako tayari kuutangaza muda wote.

“Tunataka wageni waje kwa wingi wajionee utamaduni wa wasukuma na tunaamini kuwa jambo hili litawavutia watu wengi zaidi kwani Mkoa wa Simiyu una vivutio vingi vya kitamaduni na kitalii.

Pia, ametoa wito kwa mashirika mbalimbali ya uma na binafsi yanayofanya shughuli zake katika eneo hilo kuhakikisha yanadhamini tamasha hilo ambalo litaenda sambamba na maonyesho ambayo yatawapa wadhamini nafasi ya kutangaza bidhaa na huduma zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kilimanjaro One Travel and Tours, Mohamed Hatibu amesema kampuni yake imejiandaa vizuri kuratibu tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza lakini litakuwa inafanyika kila mwaka katika Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button