Tambua viashiria vya Ukimwi kupitia mdomo
WAKATI leo dunia inaadhimisha siku ya Ukimwi, imeelezwa kuwa asilimia 50 ya watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi utaweza kuwagundua kupitia mdomo.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Afya ya Kinywa na Meno Wizara ya Afya, Dokta Baraka Nzobo, akizungumza na HabariLeo leo Desemba Mosi, 2022 amesema mdomo ndio kiungo cha awali kinachoonyesha dailili hizo mapema lakini pia asilimia 80 ya wagonjwa wa ukimwi wenye kinga mwili chini ya 200 (CD4 chini ya 200) huonyesha dalilli hizo mdomoni
“Mdomo pia unauwezo wa kutoa viashiria kwa mgonjwa wa ukimwi kama hali yake ni nzuri au mbaya kabla hata ya kufanyiwa vipimo vya maabara.” Amesema Dokta Nzobo
Amesema dalili za maambukzi ya virusi vya ukimwi mdomoni kwanza ni kupata fangasi mdomoni kwa mgonjwa wa virusi vya ukimwi ambaye hajaanza kutumia dawa za kufubaza virusi (ARV).
“Ataonyesha dalili za kuwa na utando mweupe kwenye ulimi, koo na kuta za mdomo. Utando huwa unaweza kukwangulika kiurahisi na kijiko au kitu chochote kile.
”Amesema
Amesema pia, kutokewa na vidonda kwenye kona za mdomo wa juu na chini, vidonda hivyo hutokea kama umekatwa na kitu bila kujijua,japo zipo sababu nyinginenzo zinazochangia kuleta vidonda hivyo, lakini ukiona dalili hizo nenda hospitali kapime maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
“Watu wenye maambukizi vya virusi vya ukimwi ambao wamechelewa kuanza kutumia dawa za ARV, hali ya Ugonjwa wa UKIMWI huwa mbaya na kumpelekea kupata satratani ya Kaposis Sarcoma mdomoni. Ukifika kwa Daktari wa Kinywa na Meno jambo la kwanza atakalofanya ni kukusahuri kupima kujua hali yako ya maambukizi ya VVU.
Ametaja dalili nyingine ni vidonda vyenye maumivu makali kuzunguka fizi na kuwa na utando mweupe uliooza na wakati mwingine mstari huo wa Kidonda kwenye fizi huenda kushambulia mfupa unaoshikilia meno na kuleta maumivu makali kwenye baadhi ya meno na kusababisha meno hayo kung’ooka, Mdomo kukauka. Pia vidonda ambavyo huleta homa kali na hupona vyenyewe baada ya siku 10-14.
“Uwingi wa Virusi vya Ukimwi mwilini na kupungua kwa Kinga Mwili chini ya seli 200 huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uwezo wa matezi ya mate kutengeneza na kutoa mate mdomoni. Halikadhalika moja ya madhara ya dawa za ARV ni kupunguza uwingi wa mate mdomoni.
Ndiyo maana tunashauri Mgonjwa wa UKIMWI awe anaonwa mara kwa mara na Daktari wa Kinywa na Meno ili amsaidie kumlinda na madhara yatokanayo na uwepo wa mate machache mdomoni kama vile Magonjwa ya Fizi na Meno kuoza.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 nchini ni asilimia 0.25 (kwa wanawake ni asilimia 0.34 na wanaume ni asilimia 0.17. Hii ni sawa na kusema maambukizi mapya kwa watu wenye umri kati ya miaka 15-64 nchini Tanzania ni takribani watu 72,000 kwa mwaka.
Kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 nchini ni asilimia 5.0 kwa wanawake ni asilimia 6.5 na asilimia 3.5 kwa wanaume. Hii ni sawa na kusema kwa wastani watu milioni 1.4 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaishi na virusi vya UKIMWI nchini Tanzania.
Pia takwimu hizo zinaonyesha asilimia 52 ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini Tanzania, vipimo vinaonesha
kuwa kiasi cha VVU mwilini kimefubazwa kwa wanawake ni asilimia 57.5 na wanaume ni asilimia 41.2