Tamisemi yagawa magari ya wagonjwa

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema kuwa serikali imenunua magari 528 ya wagonjwa yatakayogawiwa kwa halmashauri zote 184 nchini na kila halmashauri itapata magari mawili.

Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge waliochangia katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Kairuki alisema awali serikali ilipanga kununua magari 407 lakini baadaye ikaamua kuongeza idadi hiyo hadi kufikia magari 528 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Unicef, hivyo wameokoa magari zaidi ya 121 ambayo kama wasingetumia mbinu waliyoitumia magari hayo yasingepatikana.

Alisema kila halmashauri itapata magari mawili ya kubebea wagonjwa na gari moja kwa ajili ya usimamizi na uratibu wa miradi ya afya katika halmashauri.

Kairuki alisema tangu Aprili 7, mwaka huu magari yameanza kuwasili nchini hususani bandarini na mengine yaliwasili Aprili 14 na mengine yataingia Aprili 21 na yaliyobaki yataendelea kuja hadi yote 528 yatimie.

“Mpaka sasa yapo katika ukomboaji magari 55 zikiwepo Landcruiser hardtop 30 na ambulance 25, kikubwa kuliko yote ni kwamba kila mmoja atapata kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu,” alisema Kairuki.

Habari Zifananazo

Back to top button