WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa ametoa maagizo kadhaa kurudisha heshima ya walimu.
Bashungwa amesema ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya halmashauri kutafuta huduma na ameziagiza mamlaka za serikali za mitaa kujibu barua za walimu wanaohitaji huduma ndani ya siku saba.
Alitoa maagizo hayo Dodoma Alhamis wakati wa kuelezea mikakati ya serikali kuhudumia walimu ili kuboresha sekta ya elimu.
Bashungwa alisema serikali imekuwa ikitoa huduma kwa walimu kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao na kutoa elimu bora.
Alisema walimu wamekuwa wakipata mishahara kwa wakati na zaidi ya walimu 157,923 wamepandishwa madaraja na kurekebishiwa muundo wa utumishi.
Bashungwa alisema pia walimu 24,749 wameajiriwa katika kipindi hicho huku wanaodai malimbikizo ya mishahara wamekuwa wakilipwa na walimu wastaafu wengi wamekuwa wakilipwa mafao yao kwa wakati.
“Pia walimu wamenufaika na punguzo la Kodi ya Mapato ya Mishahara kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8 hivyo kuwapunguzia makali ya Maisha,” alisema.
Bashungwa alisema serikali itahakikisha viongozi wanasikiliza kero za walimu kuhusu madai na kuyatekeleza kulingana na sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
“Wahakikishe wanakuwa karibu na walimu, wanasimamia kupokea kero na malalamiko ya walimu katika maeneo yao ya kazi na kuzitatua ipasavyo na kwa wakati,” alisema.
Bashungwa alielekeza kuandaa mpango wa mafunzo kulingana na mahitaji na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha walimu wanaoingizwa kwenye mpango huo wanaruhusiwa na kulipia stahiki zao za mafunzo punde wanapopata udahili.
Alisema pia serikali inaendelea kuboresha vituo vya walimu kwa lengo la kuwezesha ufanyikaji wa mafunzo ya walimu kazini ili kuongeza tija katika uboreshaji wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Kuhusu upungufu wa nyumba, Bashungwa alisema serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu na kipaumbele itaanza katika maeneo ambayo ni magumu kufikika.
Alisema kwa mwaka 2022/23, Serikali imetenga Sh bilioni 55.57 kwa ajili ya kujenga nyuma za walimu ambapo ni kaya 1,916 huku alisisitiza kuwa utaratibu wa kutenga fedha utakuwa ukifanyika kila mwaka.
Bashungwa alielekeza viongozi wa elimu wa ngazi ya halmashauri kufuatilia ufundishaji wa walimu darasani na kutatua kero zao katika maeneo yao ya kazi.
“Ninaelekeza kwamba viongozi wanaowahudumia walimu waende shuleni kuwahudumia walimu, siyo kukaa ofisini peke yake,” alisema.
Kuhusu upandishwaji vyeo na madaraja kwa walimu, Bashungwa amewataka Tume kuhakikisha wanaziwezesha Kamati za Tume ngazi ya Wilaya kuwapandisha walimu madaraja, na kuwarekebishia vyeo kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.
Pia amemwelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu, kuchambua upandaji madaraja ya kila mwalimu na kuchukua hatua kuwapandisha madaraja walimu watakaobainika kucheleweshewa stahiki zao za madaraja.
Bashungwa pia aliagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, kusimamia mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi za Tume na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.
Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia watendaji wanaotoa huduma kwa walimu ili wawafuate walimu shuleni na kutatua kero na malalamiko kwa wakati.
“Pia mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa,” alisema Bashungwa.
Bashungwa pia amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia mamlaka za uteuzi wa viongozi wa elimu ili viongozi wa elimu wanaoteuliwa, wawe ni wenye weledi, uzalendo, uadilifu na wachapakazi.
Alisema pia wasimamie maofisa wa tume kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa au kurekebishiwa cheo apandishwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Bashungwa alisema serikali imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu ili kuwawezesha wanafunzi kupata umahiri unaokusudiwa kwa masomo yote.
“Niwakumbushe walimu kuwa kila mmoja wenu anao wajibu wa kujiwekea malengo yake binafsi katika masomo anayofundisha na ahakikishe hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri katika masomo anayofundisa ifikapo mwishoni mwa kila mwaka,” alisema.