Tamko la Tanzania kushusha bei ya mahindi Kenya

Tani 30 mahindi ya msaada zapelekwa Kahama

BEI ya mahindi iliyopanda kutokana na kuenea kwa uvumi kuwa Tanzania imesitisha utoaji wa vibali vya uingizaji wa mahindi nchini hapa, inatarajiwa kushuka baada ya nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mahindi yanayouzwa hapa nchini kukanusha taarifa hizo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Kenya, taarifa hizo za uzushi zilisababisha bei ya mahindi kupanda kote nchini kutoka Sh za Kenya 5,400 hadi 5,900 kwa gunia moja la kilo 90, na kusababisha unga nao kupanda bei kutoka Sh 190 hadi Sh 210 kwa kilo.

Vyombo hivyo likiwamo gazeti la Daily Nation, vimebainisha kuwa, tamko la Tanzania kukanusha taarifa hizo litasababisha unafuu na kupungua kwa bei ya bidhaa za mahindi na unga na kurudisha katika hali yake ya kawaida.

Advertisement

Wizara ya Kilimo nchini Tanzania ilisema serikali haijasitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mahindi kwenda Kenya kama taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinavyodai ikisema wafanyabiashara wote wanayo ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Kilimo, Hudson Kamoga alisema na kunukuliwa na gazeti la HabariLEO kuwa serikali na Wizara ya Kilimo zimeendelea kutoa vibali muda wote bure kwa wafanyabiashara wanaosafirisha mahindi nje ya nchi.

Alisema changamoto inayojitokeza kwa wafanyabiashara ni kupeleka mahindi hadi mpakani wakiwa hawana nyaraka zinazohitajika kuwawezesha kusafirisha mahindi nchini Kenya huku wengine wakisubiri hadi wafike mpakani ndio waanze kuomba vibali vinavyohitajika.

“Unakuta mfanyabiashara ana nyaraka zote, lakini anakosa moja, mfano unaweza kukuta mtu ana nyaraka zote lakini anakosa leseni ya BRELA (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni)

ya kuonesha usafirishaji wa nafaka ambacho ni moja ya mahitaji ya mfumo akitakiwa kuambatanisha,” alisema Kamoga.