Tamu na chungu miaka 36 ya TAMWA

“WAKATI Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kinaanzishwa mwaka 1987, kulikuwa na vitendo vingi vya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na vitendo viovu dhidi ya wanawake na watoto mfano vipigo na watoto wadogo kunajisiwa, sasa TAMWA ilivyokuja ikasema hapana hivi vitendo havifai tuviache,” hiyo ni kauli ya mmoja wa waasisi wa Tamwa, Edda Sanga katika mahojiano na HabariLEO katika maadhimisho ya miaka 36 ya Tamwa.

Edda ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, anasema kutokana na ukatili uliokithiri kwa jamii, Tamwa iliendesha kampeni kubwa ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto na kutumia wabunge wa wakati huo, akiwemo  Mariam Khan na Anna Abdallah ili kusukuma ajenda mbele.

“Tuliwaeleza wabunge nini tunataka kutoka kwao, na bunge lilikua ‘live’ kupitia Radio Tanzania,  kila walichokua wanachangia kilienda hewani, walitusaidia kujua kwa nini ilikuwa ni muhimu kwa wabunge kusaidia harakati za kupinga ukatili wa kijinsia na ubakaji.

“Tulifanikiwa kwa sababu baada ya kwenda hewani watu walisikia na walielewa ingawa kwa wakati ule wabunge hawakukubalina na sisi moja kwa moja,” anasema

Sheria ya SOSPA

Edda anasema, baada ya mashinikizo yao kwa wabunge na kukesha kwenye mahema, hatimae baada ya miezi sita sheria ya makosa ya kujamiiana na ubakaji SOSPA ikapitishwa

Anasema, lengo la sheria hiyo ni kukomesha vitendo vya ubakaji kwa watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi, ambapo pale mtuhumiwa akikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela na kesi ikihusisha watoto wenye chini ya umri wa miaka 10 mtuhumiwa akikutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha jela.

Hata hivyo, anasema katika harakati hizo,  TAMWA  pia lilikuwa inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, Bunge na jeshi la polisi katika kuleta matokeo chanya  ya harakati zao.

“Tulikuwa tunafanya nao kazi katika harakati za kuhakikisha uwepo wa sheria na sera mbalimbali zinazotambua usawa kwa wanawake na walitusikiliza na kushirikiana nasi katika kutengeneza mazingira ambayo kweli unaweza kusema taifa letu linazingatia  usawa wa kijinsia.”

Matokeo bado si mazuri

Edda anasema licha ya uwepo wa sheria hiyo ya SOSPA bado matokeo si mazuri, hayaridhishi kutokana na muathirika wa tukio la ubakaji kutakiwa kuwa na  uthibitisho kuwa mtu huyu kabakwa na apelekwe mahakamani.

“Ninavyoona  jamii imekua ngumu sana kufuatilia kwa sababu vitendo hivi vimekuwa vikifanyika ndani ya jamii wa hiyo wanaogopa kuumbuana, hawaelewi yule aliyefanyiwa ukatili ndio anazidi kuumia kwa kumtetea mhalifu asiathirike.

“Bahati nzuri kwa sasa vyama vinavyotetea wananchi vipo vingi hatupo peke yetu, na si wanawake tu hata wanaume wanatendewa ndivyo sivyo, ila elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa jamii,” anasema.

Zanzibar ukatili ulikithiri

Kwa upande wa Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar , Mzuri Issa anasema waliamua kufungua ofisi Zanzibar kwa ajili ya kuchagiza harakati za kupigania haki za watoto na wanawake na kwamba ukatili wa kijinsia ulikuwa mkubwa na haukua ukiripotiwa.

Anasema  utafiti tuliofanywa na TAMWA  2002 hakukua na  kesi hata moja  iliyokua imeripotiwa na mahakama kumtia hatiani muhusika.

” Toka tulipoanzisha ofisi, mwaka 2003 maendeleo makubwa yameanza kufikiwa, kesi zilizokuwa haziripotiwi zikaanza kuripotiwa, baada ya kuanza kutoa elimu kwa jamii, kwenda kuzungumza na waathirika na kuwashawishi kwenda mahakamani sio kumaliza ngazi ya familia, ” anasema Mzuri.

Anasema, kulikuwa na sheria ngumu kwamba ili hatua zichukuliwe ni lazima kuwe na mashahidi wanne walioona hilo tendo linatendeka, ilikuwa ngumu kupata ushahidi kwenye kesi kama hizo.

“Yani ilikuwa ni heri kuachiwa huru watu 99 kuliko kumfunga mtu mmoja kwa kesi ambayo haina ushahidi. Mafanikio makubwa kwa sasa tangu mwaka 2010 kesi zimeanza kupata hukumu, ” anasema.

Anasema, takwimu za mwaka jana kesi 111 zilipata hukumu ni sawa na asilimia 13 ya kesi zote zilizoripotiwa.

Anasema sheria ya ushahidi imerekebishwa 2016 hakuna haja ya mashahidi wote ni cheti cha daktari na muathirika mwenyewe ndio maaana kesi imeongelewa. Pia, Mahakama za wilaya zimepewa nguvu za kuhukumu hata miaka 15.

Kwa upande wa Rose Haji ambae ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho anasema kulikuwa na mtu anaitwa Maumba, kazi yake likuwa kubaka na kulawiti watoto wa shule, maeneo ya Kisutu, baada ya kujua TAMWA  haikukaa kimya ilipigiwa kelele akashtakiwa na kufungwa.

“Tulikuwa hatuna pesa, tuliweka kambi mahema tunalala pale na baridi tulikaa siku saba tukisubiri kupitisahwa sheria ya SOSPA.

“Uendeshaji mashtaka mifumo inabadilika, mfano mtoto kabakwa sasa akipelekwa hospitali, milolongo mingi, vikwazo vingi,  siku ya kutoa ushahid, ” anasema

Aidha, anasema madawati ya kijinsia kwenye vituo vya Polisi ni matunda ya TAMWA  kama sio sheria ya SOSPA madawati hayo  yasingekuwepo.

Naye, Mkurugenzi wa Tamwa Bara, Rose Reuben anasema ktika safari ya TAMWA ya miaka 36 iliweza kuanzisha gazeti la Sauti ya Siti, lililoibua masuala ya uchunguzi na utafiti na Makala hizo ziliandikwa na waandishi wanawake na wanaume.

“Kadiri siku zilivyokwenda watu binafsi, taasisi, asasi, serikali na wadau wengine walianza kuunga mkono jitihada za TAMWA, kupiga vita ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia,”amesema.

Sheria ya wanawali kufutwa

Rose anasema  kuondolewa kwa sheria ya wanawali mwaka 1985,  ambapo msichana akipata mimba alifungwa jela na kama ni mwanafunzi hakuruhusiwa kurudi tena kusoma shule.

“Sheria hii iliondolewa kwa jitihada na ushawishi wa Rais Samia Suluhu Hasan, ambaye kwa wakati huo alikuwa Waziri wa Zanzibar anayeshughulikia dhamana ya masuala ya kijinsia, alibeba tatizo hilo hadi hatimae ile sheria ikafutwa,”amesema Dk Rose.

Aidha, amesema TAMWA inaendelea kutumia vyombo vya habari kuhamasisha na kushawishi ili kuwatia moyo wanawake na vijana waliokuwa tayari kugombea nafasi za kuchaguliwa za kisiasa.

“Mafanikio ya TAMWA hayapo katika kutekeleza miradi tu lakini pia tunajivunia kuwapa elimu wanahabari hapa nchini pamoja na kuhamasisha kuwekwa kwa sera ya jinsia ndani ya vyombo vya habari,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button