WAKATI dunia ikiadhimisha siku ya wanawake leo Machi 8,2023 Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) kimesema bado Kuna mapengo kadhaa yanayoibua changamoto za usawa wa kijinsia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa Rose Reuben amesema leo Machi 8,2023 kuwa Tamwa inaamini katika kuibua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wa kike, kuhamasisha kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, na kuwapongeza wanawake na watoto wa kike, waliofanya vyema katika jamii yetu.
Teknolojia ikiwamo mitandao ya kijamii, itumiwe vyema kuibua madhara ya ukatili wa kijinsia na habari potofu mtandaoni , kuasa juu ya vitendo vya udhalilishaji na zaidi kuonyesha fursa zinazokuja na ukuaji wake kwa nafasi ya wanawake na wasichana katika jamii.
Amesema, utafiti uliofanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebaini kuwa, asilimia 79 ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2020.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, uchaguzi mkuu wa 2020 umeonekana kama moja ya nyakati ambapo idadi kubwa ya wanawake katika siasa walikabiliwa na unyanyasaji wa mtandaoni, hasa wale wa nafasi za viti maalum 19 vya upinzani ambao walipewa majina na kudhalilishwa mtandaoni kwa muda mrefu.
‘Ni dhahiri kuwa teknolojia imeleta neema lakini wakati mwingine, inatumiwa vibaya na kusababisha madhara kwa makundi mbalimbali hasa wanawake.”Amesema
Amesema, jamii inapaswa kuzitambua na kuzitumia fursa mbalimbali zinazokuja na tekknolojia kama vile biashara, ajira, mawasiliano rahisi na kwa kutumia fursa hizo ichagize ubunifu na maendeleo kwa mlengo wa usawa wa kijinsia.
“Wakati tunaendelea na kumbukizi za Siku ya Wananawake Duniani TAMWA tunawakumbusha Wanawake na wasichana wanaotumia teknolojia, wazitumie kwa manufaa.” Amesema na kuongeza”
Wawekeze na endapo wanashambuliwa au kudhalilishwa kwa namna yeyote wachukue hatu za haraka kutoa taarifa katika vyombo vya usalama ili waweze kusaidiwa na kulindwa dhidi ya ukatili huo kabala ya kupatwa na madhara makubwa.
“Kama wachapishaji wa jarida la Sauti ya Siti, tuliweza kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii na tukafanikiwa kwa kutumia fasihi andishi, tunaamini pia, fasihi hiyo hiyo ikitumika vyema kidijitali, itamuinua mwanamke na msichana wa kitanzania.” Amesema Dk Rose
m
Amesema, TAMWA inaamini katika nguvu chanya ya teknolojia, na inatamani wanawake na wasichana waitumie kwa ubunifu ili waweze kujikomboa kijamii, kiuchuni na kisiasa.
“Ni wakati sasa wa kuongeza maarifa kwa matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kijinsia ili tuwe na taifa lenye usawa.” Amesema