Tamwa yainyooshea kidole Sheria ya Mahakama ya Kadhi

Mkurugenzi wa Tamwa, Zanzibar, Dk Mzuri Issa

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA – ZNZ) kwa kushirikiana na asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu leo wanaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuwasilisha ripoti ya upungufu uliopo katika sheria ya Mahakama ya Kadhi.

Mahakama ya Kadhi ndiyo inayosimamia masuala ya mirathi na talaka kwa lengo la kupatikana kwa sheria moja ya Kiislamu itakayosimamia masuala ya kifamilia na itakayotoa haki na usawa kwa wanawake na watoto.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Tamwa, Zanzibar, Dk Mzuri Issa alisema maadhimisho hayo yatafanyika katika ukumbi wa Zura na yatahusisha washiriki kutoka taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya kisheria, haki za binadamu na wana mtandao wa kupinga vitendo vya udhalilishaji.

Advertisement

“Miongoni mwa sheria ambazo zimepitiwa na kuonekana kuwa zina mapungufu ni Sheria ya Mahakama ya Kadhi Na.9 ya mwaka 2017, Sheria ya Mufti Na 4 ya mwaka 2021, Sheria ya Wakfu na Mali Amana ya mwaka 2007, na Sheria ya mtoto Na. 6 ya mwaka 2011,” alisema Dk Mzuri.

Alisema sheria hizo zinaonekana kuwa na upungufu unaowanyima haki wanawake na watoto hasa katika suala la mgawanyo wa mali, haki ya mwanamke baada ya talaka na matunzo ya watoto baada ya kuachana na kuwafanya watoto kukosa haki zao za msingi ikiwamo haki ya kulindwa, kupata elimu na kuongeza idadi ya watoto wa mitaani kwa kukosa malezi bora ya wazazi.

Aliongeza Sheria ya Wakfu na Mali ya Amana haikuweka bayana kuhusiana na mirathi na hivyo kufanya mirathi kuchelewa kugawiwa kwa wahusika hali inayosababisha kukosa haki mapema na kulazimika kukatisha ndoto zao kama vile kuwapatia elimu watoto wao.

“Licha ya changamoto zilizoko katika sheria hizo juu ya haki za mwanamke, ziko sheria ambazo zimetambua nafasi ya mwanamke katika mambo mbalimbali.

Mfano Sheria ya Mahakama ya Kadhi Namba 9/2017, Kifungu cha 5(1)(f) ambacho kimewapa nafasi wanawake kupeleka malalamiko yao juu ya ugawaji wa mali.

Alisema sheria ya Mahakama ya Kadhi haimsaidii mwanamke kwani bado utekelezaji wake unafuata matakwa ya Kadhi mwenyewe kwenye sheria hiyo.

Alisema katika kipindi cha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia zikiadhimishwa duniani kote, bado kuna changamoto nyingi zinazowaandama wanawake na watoto ikiwamo kuendelea kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vinayochangiwa na kutokuwapo kwa mifumo imara ya kuwalinda na kuwapatia haki waathirika kwa wakati mwafaka.

Dk Mzuri alisema kaulimbiu ya asasi hizo mwaka huu ni ‘Tuungane kumaliza vitendo vya udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia’ na kaulimbiu hii inakwenda sambamba na kaulimbiu ya kitaifa isemayo ‘Tuungane kumaliza ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto’.