Tanapa, TTB waguswa tuzo Serengeti, Tarangire
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) wamesema tuzo walizopata hifadhi za taifa za Serengeti na Tarangire zitakuwa na manufaa kwa sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Damas Mfugale alisema tuzo hizo ni nyenzo ya kimasoko itakayowezesha kupaa kwa soko la utalii hasa eneo la uhifadhi wa wanyamapori.
Hifadhi hizo zimepata Tuzo za Chaguo la Wasafiri kipengele cha kivutio bora kati ya vivutio bora vya juu Afrika. “Zitapaisha mustakabali wa sekta ya utalii, kama Serengeti na Tarangire wamepata tuzo hata wale wasafiri wanapata nafasi ya kuchagua kuja Tanzania kwa sababu dunia imetutambua,” alisema Mfugale.
Alisema kwa kadri Tanzania itakavyoendelea kupokea tuzo, itasaidia kupaa kwa sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla.
Mfugale alisema Tanzania iko vizuri katika uhifadhi wa wanyamapori ndiyo sababu tuzo kama hizo zinatolewa hasa ukizingatia kuwa kwa sasa Tanzania inatambulika kwenye Tume ya Safari na Utalii Duniani (WTTC).
Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, William Mwakilema alisema tuzo hizo zinatolewa na mtandao wa Tripadvisor unaojihusisha na kutangaza vivutio vya utalii na utamaduni na kusaidia wasafiri kuvifikia vivutio hivyo na baadaye kukusanya maoni yanayowezesha kupatikana kwa tuzo hizo. Kamishina Mwakilema alisema tuzo hizo zilipatikana kutokana na maoni ya watalii ambao walitembelea mbuga hizo na kuvutiwa na kile walichokiona.
Alisema filamu ya ‘The Royal Tour’ imechangia kupatikana kwa tuzo hizo kwa kuwa ilisaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini. Mwakitelema alisema kupatikana kwa tuzo hizo kutaendelea kuzitangaza hifadhi hizo kwa kuwa mtandao huo unatembelewa na watu wengi duniani.
“Mtandao unapitiwa na watu wengi duniani, inasaidia kuongeza mapato ya kigeni, kwa sasa utalii unachangia asilimia 21 ya mapato ya kigeni hivyo itasaidia kupaa kwa uchumi,” alisema. Kwa mujibu wa Tripadvisor, vigezo vinavyotumika kupata washindi wa tuzo hizo ni pamoja na kivutio kuwa katika orodha ya mtandao huo kwa miezi 12.