Tanesco: Hakutakuwa na shida ya umeme SGR

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema hakutakuwa na tatizo la umeme kwenye treni ya Reli ya Kisasa (SGR).

Mhandisi wa Idara ya Mipango Tanesco, Lucas Magero amesema mradi wa SGR utatumia umeme wake peke yake hivyo hakutakuwa na kukatikakatika.

Magero alisema hayo Dodoma jana kwenye mabanda ya Wizara ya Nishati katika maonesho ya Wiki ya Nishati.

Alisema Tanesco ina miradi mikubwa kwenye gridi ya taifa na wanatarajia kuzalisha megawati 2,000 zitakazotosha kwenye SGR ambayo makadirio yao ni kutumia megawati 416.

“Kwa sasa mradi wa SGR sehemu ya Dar es Salaam mpaka Morogoro umekamilika kwa asilimia 100… na kutoka Morogoro mpaka Makutupora imekamilika asilimia 99. Kutoka Isaka mpaka Mwanza ndio tumepata mkandarasi na ataanza kazi Juni,” alisema.

Aliongeza: “Bwawa la Nyerere likianza, kila kitu kitakuwa sawa na hakutakuwa na kukatika umeme kwenye treni, hata kama ikitokea changamoto treni itakuwa na uwezo wa kutembea kilomita 50 bila umeme.”

Mradi wa kuzalisha umeme kwa maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ni miongoni mwa miradi ya mkakati ya Tanesco utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115.

Katika maonesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema kupitia JNHPP nchi ipo kwenye mikono salama.

Simbachawene alisema kiwango cha maji kitakachojazwa kwenye bwawa hilo litakapokamilika litafanya nchi isahau tatizo la umeme.

“Nawapongeza sana Tanesco, imekuwa sekta ya ukombozi wa uchumi wa nchi…suala la uzalishaji umeme lilikuwa gumu tangu enzi na enzi. Bwawa la Nyerere tangu Rais Samia (Suluhu) azindue ujazo wake wa maji ni mara nne ya lile la Mtera na hapo halijaisha,” alisema.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde aliipongeza Tanesco kwa ubunifu wa JNHPP kwa kuwa litakapokamilika nchi itajikomboa kiuchumi.

Mavunde alisema ana matarajio makubwa kwa wananchi kupata umeme wa uhakika na viwanda kujiendesha bila tatizo la nishati hiyo.

“Wizara ya Nishati ifikirie kufanya maonesho haya Tanzania nzima ili Watanzania wajionee miradi inavyokwenda, waone namna serikali inavyofanya kazi zake kupitia Wizara ya Nishati,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button