Tanesco Mtwara watakiwa kuelimisha wananchi

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya, amelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Mtwara, kutumia wiki ya huduma kwa wateja, kuelimisha wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo na  namna bora ya kuzipeleka kwa wananchi kwa haraka.

Kyobya ametoa agizo hilo leo wakati akizundua utoaji wa huduma hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, huku akisema Mkoa wa Mtwara, una umeme wa kutosha.

Kyobya amesema changamoto kubwa ni wananchi kutokuwa na uelewa sahihi wa namna ya kupata huduma hizo, pamoja na  miundombinu ya umeme kuwa mibovu.

“Tanesco tumieni wiki hii kuelimisha wananchi kuhusu huduma za umeme, tafuteni na kujua kero  ambazo wananchi wanakumbana nazo, pia tangazeni mfumo mpya wa Tanesco wa kuhakikisha huduma kwa wateja kwa haraka,” amesema.

DC huyu amesema matumizi ya umeme Mkoa wa Mtwara ni megawatt 15 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa ni megawatt 25 mpaka 30 kwa siku.

Meneja Tanesco Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Tawakali  Rwahila, amesema serikali imetoa sh bilioni nne mwaka huu wa fedha, kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya umeme na kuongeza nguvu ya umeme mkoani humo.

Habari Zifananazo

Back to top button