SERIKALI imesema haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu ambaye atahujumu taswira ya nchi kupitia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba alisema hayo Alhamis wakati akifungua kongamano la fursa zikiwamo huduma, biashara na ajira zinazotokana na mradi wa bomba hilo kwa wafanyabiashara waliopo ndani na nje ya Mkoa wa Tanga.
Mgumba alisema serikali haitakuwa tayari kuona mradi huo unatekelezwa chini ya kiwango kwa makusudi kinyume cha mkataba na makubaliano yaliyopo kwa lengo la kuuhujumu.
“Serikali za nchi zote mbili zina matumaini makubwa na mradi huu kwamba utakapokamilika utasaidia kuinua uchumi wa watu wake na nchi hizo kwa ujumla,” alisema.
Mgumba alisema ana imani watu ambao watapata fursa ya kushiriki kazi kwenye mradi huo watafanya kazi zenye ubora na viwango ili ulete matokeo mazuri.
“Rai yangu kwa watu wote ambao wataweza kupata fursa ya ajira kupitia mradi huu wa bomba la mafuta, kuhakikisha wanafanya kazi kulingana na kanuni na taratibu ambazo wamekubaliana badala ya kufanya hujuma na pia natoa wito kwa vijana na wanawake kuchangamkia fursa hizo za ajira,” alieleza.
Aidha, alisema mradi huo kwa Mkoa wa Tanga pekee unatarajia kuzalisha fursa za ajira zipatazo 800 ambazo ni rasmi na zisizo rasmi hivyo aliwataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo.
Mratibu wa Mradi wa Bomba la Mafuta Kitaifa, Asiad Mrutu alisema tayari maandalizi ya ujenzi wa mradi huo yamekamilika kwa kiwango kikubwa.
Alisema kuwa upande wa eneo la Chongoleani ambako kutajengwa miundombinu ya matangi ya kuhifadhi mafuta, kwa sasa watafiti wanaendelea na kutafiti udongo ili kujua tabia zake kabla ya kuanza ujenzi wa matangi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema alisema takribani asilimia 52 ya mradi huo ipo mkoani humo hivyo wananchi wategemee fursa lukuki za ajira.
Alisema jumla ya nyumba 49 zinakwenda kujengwa kwa wananchi ambao wamepisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, huku takribani Sh bilioni 1.2 zimelipwa kwa ajili ya malipo ya fidia kwa kaya 120.