TANGAUWASA yakusanya Sh bilioni 54.7 mauzo hatifungani

TANGA: Mamlaka yetu ya Maji Tanga (TANGAUWASA) imefanikisha mauzo ya asilimia 103 ya Hatifungani ya Kijani ya miundombinu ya maji Tanga ambapo zaidi ya Sh Bilioni 54.72 zimekusanywa.

Akitoa pongezi zake kwa TANGAUWASA, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema fedha hizo zimekusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa matarajio yalikuwa ni kukusanya Sh bilion 53.12.

“Kwa hili tumevuka lengo na haya ni mafanikio makubwa sana. Hili ni wazo la Mhe Rais Samia_Suluhu_Hassan na mnamo Feb 22, 2024 aliwakilishwa na Mhe Makamu wa Rais Dkt Philip Mpnago katika uzinduzi wake,”amesema Aweso.

Advertisement

Amesema kwa sasa wapo hatua ya matokea na mauzo na hatua nyingine zitafuata.

“Haya ni mapinduzi makubwa katika sekta yetu ya maji yenye lengo la kufanikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, kwa hakika sekta ya maji imeandika historia mpya Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ubunifu huu,”amesema.

Aidha, Aweso amesema awali jambo hilo lilionekana haliwezekani lakini aliwasisitiza uthubutu na wameweza.
Amesema, fedha zilizopatikana zinaenda kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimakakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Tanga Jiji pamoja na Miji ya Muheza, Pangani na Mkinga sambamba na kuimarisha usimamizi na utunzaji wa vyanzo vya maji.