‘Tangulizeni maslahi ya wananchi kuwaletea maendeleo’

MBUNGE wa Rufiji, ambaye pia ni Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amewataka madiwani wa Rufiji kutanguliza mbele maslahi ya wananchi wakati wa kufanya uamuzi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza  katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Rufiji kujadili taarifa ya ugawaji wa ardhi ya Rufiji kwa wawekezaji, Mchengerwa amewaomba kuangalia maslai ya wananchi.

“Niwaombe  tutangulize maslahi ya wananchi wa Rufiji kama miradi tunakwenda nao tunasema utatuwezesha kuwapatia ajira wananchi wetu zaidi ya 10,000 hatuna sababu ya kumkataa mwekezaji,” amefafanua  Mchengerwa wakati alipokuwa akizungumzia mradi wa uzalishaji wa sukari.

 

Mradi huu wa uzalishaji sukari unafanywa na mwekezaji Lake Group ni mradi wa pili kwa ukubwa hapa nchini kwa uzalishaji wa sukari ukiondoa ule unaotekelezwa wilayani Bagamoyo.

Ameongeza kuwa kuhoji na kufahamu vizuri miradi mbalimbali inayofanyika katika kipindi hiki kutawafanya wawe mabalozi wazuri wa kuisemea serikali maendeleo makubwa yanayofanyika, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuwaletea maendeleo wanarufiji na Watanzania kwa ujumla katika kipindi kifupi.

Katika siku za hivi karibuni, Mchengerwa alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vyote vinavyoguswa na mradi huo na kujadiliana nao, ambapo walikubaliana na mradi huo kwa kauli moja huku wakitaka mwekezaji kuja kujadiliana  nao badala ya kuwa na uwakilishi wakati wa vikao miongoni mwao.

Wakati huohuo Kaimu Mwenyekiti  wa Baraza hilo, Ally Ndungutu amemshukuru Mchengerwa kwa kumaliza mgogoro huo, baada ya kuamua kuja kwa wananchi wanaozunguka katika mradi huo na kuwasiliza kero zao.

Habari Zifananazo

Back to top button