Tani 300,000 za mbolea zinatumika kwa mwaka

TANZANIA imekuwa ikitumia kati ya tani 300,000  hadi 600,000 za mbolea aina mbalimbali kwa mwaka na hiyo ni sawa na asilimia 30 hadi 60 ya lengo ambalo ni tani milioni 1 kwa mwaka.

Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mkoa wa Morogoro, Dk Rozalia Rwegasira alisema hayo mjini Morogoro akifungua mafunzo ya udhibiti ubora wa mbolea nchini.

Mafunzo hayo yaliratibiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na kushirikisha  washiriki 20 kutoka Sekretarieti za mkoa na Mamkala za Serikali za Mitaa.

Advertisement

Mikoa hiyo ni  Arusha, Dar es Salaam, Dodoma , Kigoma , Kilimanjaro, Manyara , Morogoro, Mwanza , Njombe , Simiyu, Singida , Tabora na Rukwa.

“Katika miaka mitano iliyopita Tanzania imekuwa ikitumia kati ya tani 300,000 na 600,000 za mbolea aina mbalimbai kwa mwaka. “ alisema Dk Rwegasira.

Dk Rwegasira alisema mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea kwa sasa umekuwa na umuhimu wa pekee hasa ikizingatiwa serikali ya awamu ya sita imetenga bajeti ya ruzuku ya mbolea kwa wakulima kuanzia msimu wa mwaka 2022/2023 na msimu wa 2023/2024.

Alisema kuwa hatua hiyo imewezesha wakulima kupata na kutumia bolea bora kwa gharama nafuu .

Dk Rwegasira, alisema juhudi hizo  za serikali zinalenga kuongeza tija ya uzalishaji , kuimarisha usalama wa chakula, kuwezesha upatikanaji wa malighafi za viwanda , kuwezesha ukuaji wa sekta ya kilimo na kuimarisha uchumi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA , Joel Laurent, katika  hotuba yake iliyosomwa na Meneja wa Uhusiano ,Mawasiliano na Elimu wa Mamlaka hiyo ,Matilda Kasanga alisema kwa mujibu wa sheria ya mbolea ,mamlaka imepewa majukumu ya kusimamia ubora wa mbolea.

Joel alitaka majukumu hayo ni pamoja na kudhibiti ubora wa utengenezaji, uingizwaji, usafirishaji nje ya nchi , uuzaji na utumiaji wa mbolea hapa nchini .

Alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kusimamia ubora na kufanya ukaguzi kudhibiti ubora wa mbolea na usimamizi wa mfumo wa Ruzuku ili kuimarisha upatikanaji wa mbolea bora kwa wakulima itakayowawezesha kuongeza uzalishaji na tija.

Alitaja, eneo lingine ni kufahamu sheria ,kanuni na taratibu zinazotumika katika tasnia ya mbolea nchini , mfumo wa kidijitali wa usambazaji wa mbolea ya Ruzuku.

Joel aliwataka wakati wote wa majukumu yao wakiwa wakaguzi wa mbolea kutenda haki ili kuhakikisha biashara ya mbolea inafanyika katika mazingira wezeshi kwa pande zote .

Nao wahitimu wa  mafunzo hayo , Upendo Chaula kutoka Jiji Mwanza pamoja na Evetha Lyatuu kutoka  halmashauri ya Mji wa Babati , kwa nyakati tofauti walisema mafunzo yao yamewajengea uwezo mkubwa tofauti na hapo awali.

Chaula alisema pamoja na kufanya ukaguzi wa mbolea , pia watashiriki utoa  elimu kwa wakulima watumie matumizi sahihi ya mbolea kwa kupata ushauri kutoka kwa maofisa ugani waliopo maeneo yao ya uzalishaji ili kupata mavuno yenye tija.

1 comments

Comments are closed.

/* */