SERIKALI imeruhusu kuingizwa nchini kwa tani 50,000 za sukari kwa mwezi wa Januari na Februari kama njia ya kutatua tatizo la uhaba wa sukari nchini.
Waziri wa Kilimo, Hussin Bashe amesmea hayo na kueleza kuwa kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini kimeshuka kuanzia Novemba 2023 kutokana na mvua nyingi zinazonyesha na kusababisha kushindwa kuunwa kwa miwa mashambani mwaka huu.
“Pamoja na mvua kuendelea maeneo ya uzalishaji, viwanda vyote vinaendelea kuzalisha. Tutaendelea kuangalia uzalishaji unavoenda na niwahakikishie walaji hali hii ndani ya siku 30-60 itatulia. Ninatambua baadhi ya maeneo bei imepanda sana niwahakikishie hali itarejea kama zamani,” alisema waziri Bashe.
Akifafanua alisema kuwa kwa miaka mitatu iliyopita uzalishaji wa ndani wa sukari umekuwa ukiongezeka na matarajio ya serikali yalikuwa kufikia tani 550,000 mwaka huu.
“Mwaka huu tungefikia lengo la kujitegemea ikiwa changamoto za muda za mvua zitatatuliwa,” aliongeza.
Aidha, alisema mahitaji ya sukari nchini ni tani 460,000-550,000 na hadi Novemba 2023, viwanda vilipunguza uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 30 na kusababisha ongezeko la bei ya sukari.